Na MWANDISHI WETU
LICHA ya kuwepo kelele nyingi za mashabiki wa Simba ambao hawafurahishwi na mwenendo wa timu zao, lakini Kaimu Kocha Msaidizi wa Wekundu hao wa Msimbazi, Selemani Matola amewatuliza na kuwaomba Wanasimba kutuliza vichwa vyao na warejeshe ushirikiano wa kuisapoti timu yao.
Matola amerejea katika kikosi cha kwanza baada ya Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira’Robertinho’ kufungashiwa virago vyake kutokana na matokeo mabovu aliyopata dhidi ya Yanga ya mabao 5-1 wikiendi iliyopita.
Kocha huyo amewatuliza na kuwaomba wanachama na mashabiki wa timu hiyo, kurejesha ushirikiano na kuendelea kuwapa sapoti na kuachana na matokeo yote waliyopata katika michezo ya nyuma.
Matola, amesema hakuna Mwanasimba ambaye hakuumia na matokeo ya kufungwa 5-1 na Yanga, bali inatakiwa kusahau kipigo hicho.
Amesema kuwa hayo ni matokeo ya mpira ambayo yanaweza kutokea wakati wowote, aliwaomba wapenzi wa klabu hiyo, kusahau yaliyopita na kujipanga upya.
Matola, amesema ameongea na wachezaji na wamemhakikishia katika michezo ijayo watajitahidi kupata matokeo mazuri.
“Kilichotokea kimetokea, tugange yajayo. Huu ni mpira na matokeo mabaya huwa yanatokea, kila mtu ameumia lakini kama ilivyo mikakati yetu ya ‘Nguvu Moja’, basi tuendelee kushikamana sababu tunayo nafasi ya kutwaa ubingwa.
“Ninawaomba mashabiki wetu waendelee kuipa sapoti timu, ninaamini tukishirikiana tutafikia malengo yetu, ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu,” amesema Matola.
Amesema kwa sasa wameanza maandalizi ya kujiandaa mchezo wa kwanza wa hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL) dhidi na ASEC Mimosas ya Ivory Coast, utakaochezwa Novemba 25, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Aidha, amesema wanajua wapinzani wao ni wazuri, wanajiandaa vyema kuhakikisha wanapata ushindi katika uwanja wa nyumbani na kuanza vyema kampeni za kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.
“Tunakutana na mpizani mgumu na mwenye kikosi bora, tunaamini tutafanya vizuri, maandalizi tumeanza sasa kila mchezaji anatambua umuhimu wa kuanza vizuri mashindano hayo katika hatua ya makundi,” amesema.
Simba imepangwa Kundi B pamoja na ASEC Mimosas, Jwaneng Galaxy (Botswana) na Wydad Casablanca (Morocco)
