Mombasa
GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, amepata pigo baada ya Bunge la Kaunti kukataa kumwidhinisha afisa mkuu mteule wa Idara ya Kawi na Mabadiliko ya Tabianchi.
Gavana alikuwa amemteua Bw John Kiprop kwa nafasi hiyo lakini madiwani wengi wamemkataa wakishangaa aliteuliwa aje licha ya kutofahamu mengi kuhusu wadhifa huo wala kuhusu Kaunti ya Mombasa.
Madiwani hao ambao wengi ni wanachama wa ODM, walisema Bw Kiprop si mzaliwa wa Mombasa, hakusomea wala kulelewa kaunti hiyo, hajui Kiswahili na si mwanachama wa upinzani.
Kwenye mdahalo mkali katika bunge la kaunti, baadhi ya madiwani walisema wameshangazwa na hatua ya mtu mwenye utajiri wa Tshs 820 milioni kusaka ajira aina hiyo Mombasa.
“Bw Kiprop alizaliwa Baringo mnamo 1974. Hajawahi kuishi, kusomea, wala kufanya kazi hapa Mombasa kwa mujibu wa sakabadhi alizowasilisha. Alipopigwa msasa hakuonyesha uhusiano wowote na Mombasa. Angekuwa mzaliwa ningemuunga mkono lakini kwa sababu ya hayo ninampinga,” akasema diwani wa wadi ya Port Reitz, Bw Fadhili Makarani.
Mwenzake wa Chaani, Bw Franklin Makanga, alisema mteule huyo hajui Kiswahili ambayo ni lugha inayotumiwa zaidi Mombasa, na pia hajui mitaa ya mji huo.
“Hajui Changamwe, Chaani wala Bangladesh iko sehemu gani. Ataleta mabadiliko gani hapa Mombasa? Hafai na ninaomba bunge hili lisimpitishe,” akasema.
Diwani wa Shanzu, Bw Allen Katana, hakuficha hitaji la kaunti kupeana nafasi za ajira kwa wafuasi wa upinzani ambao walichagua viongozi wengi wa kaunti kutoka kwa gavana hadi madiwani.
Kulingana naye, sawa na jinsi serikali ya kitaifa iliamua nafasi nyingi za kazi ziendee wafuasi wa Kenya Kwanza, serikali ya kaunti inafaa pia kuwatunuku wafuasi wa upinzani walioichagua mamlakani.
Diwani wa Kadzandani, Bi Fatma Kushe, aliwataka madiwani kufanya uamuzi huru kuhusu watu wanaoteuliwa.
“Kama mtu hafai, hafai. Tusiogope mtu yeyote, ” alisema Bi Kushe.
Hata hivyo, madiwani wachache walimuunga mkono Bw Kiprop.
Diwani wa wadi ya Kipevu, Bi Leila Nyache, alisema aliteuliwa kwa sababu amehitimu.
Mwenzake wa Junda, Bw Sylvester Kai, alisema Bw Kiprop anatoka kwa kabila la wasiokuwa wengi katika kaunti ya Mombasa kwa hivyo akipewa nafasi hiyo italeta usawa wa kikabila katika afisi za kaunti.
“Kutoka Baringo isiwe sababu ya kumnyima nafasi hii. Hakuna sheria ambayo inamzuia mtu yeyote kufanya kazi mahali kokote. Si lazima awe mkazi ama mzaliwa wa Mombasa, tuache ubaguzi, ” akasema.
Hata hivyo bunge hilo lilimwangusha.
