Daraja lililojengwa kienyeji katika wilaya ya Momba, mkoa wa Songwe hatimaye limepata ufumbuzi wa kudumu.
Daraja hilo ambalo limeshawahi kuua watu mara kadhaa kutokana na kujengwa kienyeji na kukosa uimara hatimaye limejengwa upya.
Pia, limeanza kutumika baada ya ujenzi huo kukamilika kwa asilimia tisini.
Hata hivyo, ujenzi wa daraja hilo linakadiriwa kugharimu mamilioni ya shilingi, limejengwa na mfadhili ambaye ni mzalendo wa nchi hii Bw. Ombeni Nanyaro ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM wa mkoa wa Songwe kupitia wilaya ya Momba.
Daraja hilo limeanza kujengwa mwaka jana mwezi wa saba na linatarajiwa kukamilika kabisa mwezi ujao baada ya vifaa vyote vya ujenzi kufika katika eneo la mradi.
Akizungumza na Morningstar POST, Bw. Ombeni amewaomba watu wenye uwezo wa kifedha kusaidia kutatua changamoto zilizoko vijini ili kuboresha maisha ya watu wa vijijini kwa kupitia shughuli za kilimo.
“Nawataka wafadhili wengine zaidi kusaidia maeneo mbalimbali badala ya kupenda kupiga majungu,” alisema Bw. Ombeni.
Akaongeza kwa kuwataka wakazi wa Momba kuendelea kuwa kitu kimoja katika kujenga maendeleo yao.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, Bw. Ombeni aliambatana na viongozi wa CCM kata ya Chitete, alisema kuwa daraja linaunganisha Kijiji cha Chitete na Naming’onjo.
Viongozi waliohudhuria ukaguzi wa mradi huo ni mzee maarufu Visisyla, ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Chitete, Gaudensi Siyame, Katibu wa Kata ya Chitete CCM, Bw. Gerod Simchimba.
Viongozi wa Kata ya Chitete wakiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa Songwe, Bw. Ombeni Nanyaro (wa kwanza kulia), ambaye pia ni mfadhili wa mradi huo wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.