Na BBC
Serikali ya Kenya imejitenga na madai yaliyotolewa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwamba Rais wa Tanzania Samia Suluhu alikuwa nchini humo wiki mbili zilizopita ikisema haikuwa ziara rasmi, kulingana na ripoti ya Nation Africa mtandaoni.
Akizungumza na wanahabari Msemaji wa Ikulu Hussein Mohammed alipuuza madai kwamba Rais William Ruto alikataa kukutana na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu akihoji kwamba itifaki haikuzingatiwa.
”Kila wakati rais anapozuru Kenya lazima kuna mawasiliano kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje lakini katika hali hatukupokea arifa yoyote,” ripoti hiyo ilimnukuu Hussein akisema.
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Bw. Odinga kuhusiana na suala hilo Msemaji wa Serikali ya Kenya hakutoa majibu ya moja kwa moja na badala yake alielekeza swali hilo kwa ”yule aliyesema alikuwa hapa” akiashiria Raila Odinga.
Wakati huo huo rais wa Kenya William Ruto jana Jumatano alikutana na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, siku moja baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kudai kuwa Ruto alipuuza juhudi za rais Samia kuwapatanisha kuhusu mzozo wa kisiasa wa Kenya wiki mbili zilizopita.
Marais hao wawili walikutana pembezoni mwa mkutano katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania Dar es salaam. Odinga na Ruto wametofautiana kuhusu jinsi ya kukabiliana na gharama ya juu ya maisha, sera ya ushuru ulioongezwa na pia mizozo ya baada ya uchaguzi wa mwaka jana.
Katika kikao na vyombo vya habari vya Kimataifa siku ya Jumanne, Bw Odinga alifichua kuwa Rais Suluhu alizuru Kenya majuma mawili yaliyopita lakini hakuna mawasiliano ambayo serikali ilifanya naye kuhusu jitihada za kuwaleta pamoja rais Ruto na Odinga.
Chanzo cha uhakika kutoka serikali ya Tanzania ambacho hakikutaka kutajwa jina lake kimeithibitishia BBC Swahili kuwa madai ya Raila yana ukweli.
“Rais wa Tanzania [Samia Suluhu] alikuwa nchini (Kenya)wiki mbili zilizopita. Ilikuwa ni kwa mwaliko wa [Rais] Ruto. Alibaki akisubiri. Tulikuwa tayari, lakini wao [Kenya Kwanza] hawakupatikana. Kwa kweli, ilimbidi kukaa huku kwa siku mbili,” Raila aliambia wanahabari.
Rais Samia na Rais Ruto wakiteta jambo