Mwalimu wa Mkuu wa Shule ya Msingi Kidole Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Salum Hamisi Muya, anadaiwa kutumia nafasi yake ya kazi kwa manufaa yake binafsi kinyume na sheria za nchi.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya shule hiyo mwalimu mkuu huyo Bw. Muya, amaeanzisha ujenzi wa madarasa ya shule hiyo bila kushirikisha kamati zilizoundwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo.
Licha ya kuwepo kwa kamati za mapokezi, kamati ya manunuzi na kamati ya ujenzi ya madarasa manne ambayo fedha zilitolewa na serikali Mei 27, mwaka huu shilingi milioni 80, mwalimu huyo hajatangaza zabuni ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi na bila kushirikisha wananchi na wazazi.
Hata hivyo, mwalimu huyo Bw. Muya, amekuwa akifanya ujenzi wa madarasa hayo ya shule usiku na kujenga chini ya kiwango ambapo nondo zilizotumika kujenga msingi zilikuwa nondo tatu badala ya tano.
Pia, maji yamekuwa yakinunuliwa nje ya shule wakati kuna kisima cha shule, madirisha na milango yamejengwa chini ya kiwango na ‘plastik carpet’ haikuwekwa wakati wa ujenzi wa madarasa hayo.
Chanzo cha habari cha kuaminika kinasema kuwa wakati wa ujenzi wa msingi wa madarasa mawe hayakuwekwa wakati wa kujenga jamvi la madarasa hayo na pia zabuni ya ujenzi wa madarasa hayo haikushindanishwa.
Pia, kamati ya siasa ilitoa mapendekezo kuhusu mradi huo lakini hayakutekelewa.
Mwalimu huyo Bw. Muya anadaiwa kuchangisha fedha kwa wanafunzi walioandikishwa shule kiasi cha shilingi 20,000 bila kibali chochote na idadi ya wanafunzi wa shule hiyo ni ndogo kuliko idadi ya wanafunzi iliyowasilishwa wizarani, hivyo anapokea stahiki zinazotoka wizari kwa kupotosha.
Pia, inadaiwa mlinzi wa sasa wa shule hiyo hana mkataba anatumia mkataba wa zamani na fedha zinaendelea kuingia akidaiwa akitumia kwa faida yake binafsi na hakuna jedwali la kapitesheni na ripoti ya udhibiti wa ubora shuleni hapo.
Mwalimu huyo ambaye aliwahi kufanya kazi katika shule binafsi ya Keptain Kipingu, Segerea na Lubakaya yuko katika uangalizi wa ajira ya serikali, lakini amekuwa akienda kinyume na sheria za utumishi wa umma.
Hata hivyo, mwalimu Muya, alipopigiwa simu kutoa ufafanunuzi na kujibu tuhuma hizo, alisema kwa jeuri kuwa yeye sio msemaji wa shule hiyo licha ya kuwa ni mwalimu mkuu wa shule hiyo.
“Unasemaje unashida gani? kwani kuna nini?…..kama ni hivyo mimi sio msemaji……nenda kwa msemaji”, alisema mwalimu huyo na kukata simu na alipopigiwa simu tena hakutaka kupokea tena simu.
Juhudi za kuwapata Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo na Afisa Elimu wa Wilaya kuzungumzia taarifa hizi zinaendelea.
Shule ya Msingi Kidole, iliyoko nje ya wilaya ya Ilala Dar es Salaam, maeneo ya Chanika Kidole, kwa mara ya kwanza inatoa wanafunzi wa darasa la saba mwaka huu tangu kuanzishwa.