Na Mwandishi Wetu

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kisutu, Bw Mustaquim Darugar, anadaiwa kwenda kinyume na sheria za nchi, kuikosesha serikali mapato na kunyanyasa wafanyakazi wake.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Morningstar POST, Mwenyekiti huyo wa serikali ya mtaa, anakiuka sheria za ajira kwa kushindwa kutoa mikataba kwa wafanyakazi wake kwenye makampuni yake ya ulinzi.

Pia, anadaiwa kukosesha serikali mapato kwa kuuza makampuni ya ulinzi bila kulipa kodi ya mapato (capital gain).

Pia, anadaiwa  kunyanyasa wafanyakazi wake kwa kuwafukuza kazi bila kuwalipa stahiki zao na kuuza kampuni pamoja na wafanyakazi bila kufuata taratibu.

Uchunguzi wa Morningstar POST unaonesha kuwa Bw. Darugar amekuwa akisajili makampuni ya ulinzi na kuyauza kwa watu wengine bila kufuata taratibu na kulipa kodi ya mapato (capital gain).

Kampuni zinazotajwa kusajiliwa na mwenyekiti huyo ni Simply Safe Security, Stay Alert Stay Safe Security , (ASASS), Power Sheld Security, Simply Safe Security na Thinkx GSM Security.

Kampuni ya ASASS imeuzwa kwa bwana Ali Jawadu ambaye mauziano hayo hakuna mapato ya kodi yaliyolipwa serikalini na kampuni hiyo inaendeshwa na Jawadu mtaa wa Kitonga ambako ofisi zake zilipo.

Kampuni hiyo inaendeshwa na Jawadu baada ya kununua kutoka kwa Bw Darugar.

Kampuni nyingine za ulinzi zilizouzwa na Darugar ni Simply Safe Security iliyouzwa kwa Bw Abdala, na mwingine anayefahamika kwa jina la Macho ya Paka na Almin Murtaza ambaye ni mtoto wa Bw Darugar.

Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi za Darugar waliohojiwa na Morningstar Post wameonesha wasiwasi na mashaka kuhusu ajira zao kwa kampuni kuuzwa wakati wakiwa na mikataba na Darugar.

Walisema wanashangazwa kuona mtu mmoja anasajili makampuni ya ulinzi mengi na kuyauza kama wakala na sio kampuni ya ulinzi.

Akizungumza na Morningstar POST, Meneja Rasiimali Watu, wa kampuni ya Simply Safe Security, Bw. Muhind Said alikiri kuwa kampuni hiyo inahusiana na bwana Darugar ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Thinkx GSM Security.

Alisema kuwa suala la kuuza kampuni ni kweli lakini hakutaka kuzungumzia zaidi kwa kuwa suala hilo linahusu utawala wa juu zaidi.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Simply Security anayedaiwa kuwa ni mtoto wa Darugar, alipoulizwa hakutaka kuzungumza lolote na kutaka andikiwe barua rasmi ya kuulizwa  kuhusu tuhuma hizo.

Wakizungumza kuhusu kampuni za Darugar ya Thinkx GSM Security, baadhi ya wafanyakazi ambao hawakupenda kutajwa majina yao walisema kuwa hakuna hata mfanyakazi mmoja mwenye mkataba wa ajira wala kusajiliwa kwenye mfuko wa Fidia za Wafanyakazi (WCF).

Wafanyakazi wa Darugar ambao hawana mikataba ya ajira ni pamoja na Baraka, Juma Ingo, Jeff Masabala ambao ni askari wa tahadhari (rapid rider).

Wengine ni Goshet Nyerere, Amon Rafael, Peter na Jakson ambao ni operasheni meneja. Pia, David na Shaff wataalam wa masuala ya IT, ambao hawana mikataba ya ajira.

Diwani wa Kata ya Kisutu, Khery Kessy alipoulizwa kama ameshawahi kupata malalamiko yoyote kuhusu kampuni hizo za Darugar katika mtaa wake alisema kuwa ameshawahi kulalamikiwa na wafanyakazi wa kampuni hizo na kuwashauri kwenda mahakama ya kazi au kurudi kwa mwajiri wao kupata stahiki zao.

Awali akijubu tuhuma hizo, Bw Darugar alimjia juu mwandishi wa Morningstar POST na kumtisha kuwa yeye ni mtu wa serikai yuko kwenye “system” na majina yake yako katika watu walioko ikulu anafahamika hivyo hatishwi na mwandishi.

Alisema kuhusu kampuni zake vibali vyote anavyo na ana wafanyakazi nane tu kwa kuwa yeye anahusika na kufunga alam za ulinzi tu na mikataba kwa wafanyakazi wake ipo michango ya NSSF na WCF yote anakata.

Morningstar POST ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi kuzungumzia vibali vya kampuni ya ulinzi vilivyotolewa kwa Bw Darugar bila mafanikio, lakini tunaendelea kumtafuta kuzungumzia suala hilo na kuchunguza zaidi kuhusu kampuni hizo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kisutu, Bw Mustaquim Darugar

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *