0784663087
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ametangaza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es Salaam, huku akipingana na Mganga Mkuu wa jiji hilo (DMO), Elizabeth Nyema aliyekanusha kuwa Dar es Salaam hakuna ugonjwa wa kipindupindu.
Akitangaza jijini Dar es Salaam, Ummy alisema ugonjwa wa kipindupindu umeibuka mkoa wa Dar es Salaam ambapo wagonjwa 15 walithibitika kuwa na maambukizi na hadi sasa wagonjwa 13 wamepona huku wawili wakiendelea na matibabu.
Ummy alibainisha kuwa mgonjwa wa kwanza wa ugonjwa huo alitokea katika Kata ya Kivule, Wilaya ya Ilala, Aprili 16, 2023. Alisema hadi kufikia Aprili 28, 2023 wagonjwa 15 waliotolewa taarifa, wagonjwa 13 walikuwa Wilaya ya Ilala na wagonjwa wawili Wilaya ya Kinondoni.
Hata hivyo, licha ya waziri kutangaza wiki iliyopita Aprili 27, mwaka huu Mganga mkuu wa ilala Bi. Nyema alipoulizwa na Morningstar Post alikanusha kuwa hakuna mgonjwa wa kipindupindu jiji Dar es Salaam.
Alisema wagonjwa walifika kwenye zahanati ya Kivule walikuwa wanaharisha katika hali ya kawaida.
Katika hali ya kushangaza Mganga mkuu huyo wa ilala alishindwa kufahamu taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huu licha ya kupewa dhamana ya kusimamia suala la afya katika wilaya yake.
Baadhi ya wasomaji wa Morningstar Post wamesikitishwa na kitendo cha mganga mkuu huyo kujaribu kuficha taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo.
“Viongozi kama hao hawafai katika uongozi wanatakiwa kuwajibishwa kabisa anawezaje kudanganya umma kuwa kipindupindu hakuna wakati wangojwa wameripotiwa kuwa wana kipindupindu” alisema mmoja wa wasomaji wetu kupita comment zake.
Aliwali akizungumzia kipindupindu Bi Nyema alikanusha taarifa hizo na kusema kuwa zililenga kuleta taharuki kwa wananchi wa jiji la Dar e Salaam ili watu washindwe kufanya kazi zao kwa amani na uhuru.
Bi. Nyema akawataka wananchi kuendelea kufanya shughuli zao kama kawaida kwani katika jiji la Dar es Salaam hakuna mgonjwa hata mmoja wa kipindupindu.
Hata hivyo taarifa za kuibuka ugonjwa wa kipindupindu zilisikika maeneo ya Kivule na kuwashtua baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambao kwa muda mrefu hawajakumbana na ugonjwa huo.
Licha ya Mganga Mkuu wa Ilala kukanusha taarifa za kuwepo kwa ugonjwa wa kipindupindu katika jiji la Dar es Salaam, Morningstar Post ilitahadhalisha viongozi kutodharau tetesi hizo na zichukuliwe kama chachu ya kudhibiti na kusimamia hali ya usafi katika jiji la Dar es Salaam ambalo baadhi ya maeneo hali ya usafi sio ya kuridhisha.
Katika jiji la Dar es Salaam kumekuwa na baadhi ya maeneo kuna mrundikano wa uchafu muda mrefu bila kuondolewa, maji machafu yamekuwa yakitiririka hovyo hususani katika maeneo ya katikati ya jiji.
Akizungumzia kipindupindu Ummy alisema kuwa kuanzia Aprili 24 hakuna kisa kipya kilichopokelewa wagonjwa 13 ambao wametolewa taarifa kati ya 15 wamepona, wagonjwa wawili wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri na hakuna kifo kilichotokea hadi sasa.
Ummy amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na uongozi wa mkoa huo kuhakikisha wanatibu maji kwa kutumia dawa ya klorini kwenye vyanzo vyote vya maji na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama.
“Nimemuelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na serikali ya mkoa kufanya ukaguzi wa
visima vyote vilivyochimbwa na pili kuhakikisha wanaweka dawa ya klorini kwenye vyanzo vya maji, kuchemsha maji ya kunywa kama huwezi basi tuweke dawa ya klorini,” alisema.
Ummy pia aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji, kuepuka chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyosafi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.
Tahadhari zingine ni kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula.
“Jingine ninachotaka kusisitiza ni utiririshaji wa maji taka kutoka chooni, hili lazima tulisimamie kwa kati,” alisisitiza. Aliwataka watu ambao watapata dalili za kuharisha na kutapika kuwahi haraka katika vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya saa 24.
“Kwa hiyo suala la ugonjwa wa kipindupindu kwa watu wenye dalili ni kuwahi haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa sababu mgonjwa anapoteza maji mengi kwa njia ya kutapika na kuharisha… ndani ya saa 24 anapaswa awe amefika ndani ya vituo vya huduma za afya ndio maana tunamshukuru Mungu hatuna vifo kwa sababu watu wameweza kufika kwa wakati.”
