Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Serengeti Southern Bypass – Karatu – Mbulu – Hydom – Lalago – Sibiti hadi Maswa yenye urefu wa kilometa 389 kwa kiwango cha lami.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, Aprili 30, 2026, Bungeni. Amefafanua kuwa barabara hiyo itakapokamilika itaunganisha mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa kwa njia fupi, hivyo kurahisisha shughuli za usafiri na uchukuzi nchini.

“Tayari ujenzi wa kipande cha barabara ya Hydom – Labay chenye urefu wa kilometa 25, ambacho ni sehemu ya mradi huo, umefikia asilimia 11 ya utekelezaji,” amesema Eng. Kasekenya.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali tayari imetoa fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hiyo, na taratibu za malipo zinaendelea.

Vilevile, Naibu Waziri Kasekenya amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza mradi huo, ili kuhakikisha barabara inapitika wakati wote wa ujenzi.

Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu swali Bungeni lililoulizwa na Mbunge wa Mbulu Vijijini, aliyetaka kujua ni lini barabara ya Hydom hadi Mbulu itajengwa kwa kiwango cha lami.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *