Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Italia kwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia na Zanzibar, hususan katika sekta ya utalii na maendeleo ya kijamii.
Akizungumza Ikulu Zanzibar alipokutana na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Giuseppe Sean Coppola.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuongezeka kwa safari za ndege za Shirika la ndege la Italia NEOS kutachochea ukuaji wa sekta ya utalii na kuongeza idadi ya watalii nchini.
Halikadhalika, Rais amesema Zanzibar ipo tayari kuendeleza ushirikiano wa kitamaduni, ikiwemo kuwa mwenyeji wa tamasha la muziki linaloandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania ambalo litawaleta wasanii mbalimbali kutoka Italia.
Kwa upande wake, Balozi Coppola amepongeza hatua za maendeleo zinazochukuliwa na Serikali ya Zanzibar, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, na kubainisha kuwa Jukwaa la Biashara kati ya Umoja wa Ulaya na Tanzania linalotarajiwa kufanyika Dar es Salaam litafungua fursa zaidi za uwekezaji na kukuza uchumi.