OWM – SONGWE

Timu ya wataalam kutoka Benki ya Dunia (World Bank), kwa kushirikiana na wataalam wa Serikali, imefanya ziara ya ufuatiliaji wa pamoja kukagua utekelezaji wa Programu ya BOOST katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, mkoani Songwe.

Ziara hiyo imefanyika leo Aprili 14,2026 Katika Halmashauri ya Mji Tunduma kwa lengo kujionea utekelezaji wa programu ya uboreshaji wa Elimu ya awali na msingi (Boost)

Timu hiyo imetembelea Shule ya Msingi Mpemba, ambapo wamejionea utekelezaji wa dhana ya shule salama pamoja na mbinu shirikishi za ufundishaji kwa wanafunzi wa elimu ya awali. Wanafunzi wameshiriki kikamilifu katika masomo kupitia nyimbo, michezo na mazoezi ya kuhesabu na kujifunza herufi.

Mbali na Mpemba, wataalam hao pia wametembelea shule za Makambini na Nelo, ambako wamekagua ujenzi wa miundombinu ya shule mpya za msingi unaoendelea katika maeneo hayo. Ujenzi huo ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto.

Akizungumza kwa niaba ya timu ya Benki ya Dunia, Bw. Dmitry Chigunov ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa maboresho yaliyofanyika yameleta matokeo chanya katika sekta ya elimu.

“Tumeshuhudia maendeleo mazuri, hasa katika miundombinu na ushiriki wa wanafunzi darasani. Hii inaonesha kuwa uwekezaji unaofanywa unaleta matokeo chanya,” amesema.

Kwa upande wao, Mwalimu Mkuu wa ahule ya Msingi Mpemba Mwalimu Frances Mwandosya amesema kuwa Programu ya BOOST imeleta mabadiliko makubwa, ikiwemo kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi, kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuimarika kwa ufaulu.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma Bi.Mariam Chaurembo amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 wamejipanga kukarabati zaidi ya madarasa 40 ya elimu ya awali na msingi ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira rafiki ya kujifunzia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *