Na Waandishi Wetu
JENGO moja la ghorofa lililopo barabara ya Mandela, Kata ya Tabata, Dar es Salaam lipo hatarini kuporomoka Morningstar Post inaripoti.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa hizi ambaye hakutaka jina lake lichapishwe mtandaoni, ameeleza kuwa, kuna jengo limeanza kujengwa na limechimbwa msingi uliokaribia jengo la pili na kusababisha udongo wa jengo hilo ulio chini ya msingi kuporomoka na kusababisha nyufa.
Timu ya waandishi ya Morningstar Post ilifika eneo la ujenzi na kukuta mafundi wakiendelea na ujenzi na kumtafuta Mhandisi Mkuu ili kupata maelezo yake juu ya wasiwasi huo, lakini hakupatikana eneo la ujenzi na badala yake alikuwepo Msaidizi wake anayejulikana kwa jina la Ahazi Michael, ingawa nae alikataa kuongea lolote kwa kuwa sio Msemaji wa mradi.

Aidha, waandishi walilazimika kumtafuta Mhandisi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Jeremia Mkini, ambapo alisema wanajenga Yadi ya magari na kwasasa wanashughulikia vibali.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa, ujenzi huo unaweza kuleta madhara makubwa kama wakaguzi hawatokuja kukagua kwa kuwa hata mafundi wanaojenga hawajulikani wanatoka kampuni gani kwasababu hawajaweka kibao kinachotambulisha mradi huo.
Morningstar Post inaendelea kuwasiliana na Mamlaka zinazohusika na ujenzi ili kupata ufafanuzi kuhusu suala hilo na tutatoa taarifa zaidi kwenye chapisho lijalo.