NA WAANDISHI WETU

WATUMIAJI wa pombe kali kwenye maeneo mbalimbali nchini, wapo hatarini kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya kemikali aina ya Ethanol iliyotapakaa mitaani.

Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa MorningStarPost umebaini kuwa, kwenye mitaa mbalimbali hususani jijini Dar es Salaam, kumezagaa pombe zinazotengenezwa kiholela kwa kutumia kemikali hiyo.

Imebainika kuwa, yapo maeneo ambayo ndio yameshamiri kwa biashara hiyo ya pombe ambazo zinatengenezwa bila kufuata utaratibu ikiwemo kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye ndiye mwenye jukumu la kusimamia matumizi sahihi ya Kemikali.

Kwenye maeneo mbalimbali, watumiaji wamekuwa wakiuziwa pombe kali aidha kwa kupimiwa kwenye vikombe vidogo au wamekuwa wakiwekewa kwenye chupa zilizotumika za pombe maarufu zinazotengenezwa viwandani ambazo majina yake tunayahifadhi kwasasa.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, kushamiri kwa unywaji wa pombe hizo umetokana na kupatikana kwa urahisi kwa kemikali ya Ethanol, ambayo kwenye baadhi ya maeneo waandishi walikuta idadi kubwa ya madumu yanayotumika kubebea kemikali hiyo.

Akizungumza na waandishi wetu, mmoja wa madaktari wa hospitali maarufu jijini Dar es Salaam ambaye hakupenda jina lake litoke hadharani kwasababu sio Msemaji wa hospitali hiyo alisema, matumizi holela ya kemikali hiyo yanaweza kusababisha madhara makubwa kwenye mwili wa binadamu ikiwemo kuharibu Ini.

Alisema, kuna haja kwa watanzania kupewa elimu kuhusu matumizi ya bidhaa hizo zinazouzwa mitaani na kuwasihi kulinda afya zao na kuepuka matumizi ya pombe kali kupita kiasi.

Timu ya waandishi wa MorningStarPost inaendelea na uchunguzi zaidi wa kubaini wanaohusika na utengenezaji wa pombe hizo bila kufuata utaratibu na kujua namna wanavyopata kemikali hiyo.

Mbali na hilo, waandishi wetu wanaendelea kuwasiliana na mamlaka husika kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi wa suala hilo na hatua ambazo zimechukuliwa kudhibiti matumizi holela ya Ethanol na kuzagaa kwa pombe kali zinazotengenezwa bila kufuata utaratibu na habari itaripotiwa kwa ukubwa zaidi baada ya uchunguzi kukamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *