Na Anania Njonjo
KAMPUNI moja (jina tunalihifadhi kwasasa) inayojihusisha na uuzaji wa vipuri na vilainishi vya magari ya jijini Dar es Salaam, inadaiwa kununua na kutumia risiti zinatolewa kwenye mashine za Kieletroniki maarufu kwa jina la ‘Ghost’ zinazotengenezwa na makampuni ambayo hayafanyi biashara yoyote zaidi ya kumiliki mashine za EFD na kuisababishia Serikali hasara.
Uchunguzi wa MorningStarPost umebaini kuwa, kampuni hiyo inayofanya shughuli zake barabara ya Mandela, Wilaya ya Temeke, imekuwa ikifanya mtindo huo kwa miaka mingi.
Inaelezwa, kampuni hiyo imekuwa ikinunua risiti hizo za Kieletroniki kutoka kwa kampuni mbili tofauti; moja ni OMI General Suppliers na nyingine bado mwandishi wa habari hizi anaendelea kuifuatilia na itawekwa hadharani baada ya kumalizika uchunguzi wa kubaini idadi ya kampuni ambazo zinanunua risiti hizo kwao.
Taarifa zaidi zinadai, licha ya Serikali wakati fulani kumbaini na kumchukulia hatua mfanyabiashara Mohammed Mustafa Yusuf Ali ambaye alikuwa anaiibia Serikali Matrilioni ya Shilingi kwa kutumia mashine za Kielektroniki (EFD’s) ambazo hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti bandia, bado wengine wanaendelea na mtindo huo.
Inaelezwa, makampuni yamekuwa yakinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki mashine za EFD’s ambazo nyingine zimesajiliwa ila ofisi zake hazijulikani zilipo, kisha wanazitumia kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwepo na bidhaa au huduma halisi iliyouzwa au kutolewa na muhusika, kitendo ambacho kinainyima Serikali mapato stahiki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na mwandishi wetu, mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya OMI ambayo inatajwa kuiuzia risiti kampuni hiyo ambayo jina lake tumelihifadhi, alikiri kuhusu suala hilo, ingawa aliweka wazi mara ya mwisho ni mwaka 2021.
“Ni kweli tumewahi kufanya nao biashara ya kuwauzia risiti, ila mara ya mwisho ni mwaka 2021, sasahivi nasikia wananunua kwenye kampuni nyingine ambayo sifahamu jina lake,” alisema mfanyakazi huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
Alisema, kwasasa kampuni yao imefungwa na haifanyi tena kazi hapa nchini, ingawa wamefanya shughuli hizo kwa miaka mingi na wamewauzia risiti wafanyabiashara wengi wenye makampuni makubwa jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa habari hizi, alimtafuta Mhasibu wa kampuni hiyo Tejal Kanji ili kujibu tuhuma zinazowakabili za ununuzi wa risiti hizo, lakini mara zote amekuwa akipiga danadana kujibu tuhuma hizo, ingawa bado jitihada za kufuatilia ili kupata ukweli wa tuhuma hizo zinaendelea.