MKUU wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema maonesho ya mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa yameonesha kwa vitendo utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), hasa katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Akizungumza kwa niaba ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Morogoro, Mhe. Kunenge amesema maonesho hayo yameakisi vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza tija kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.

“Maonesho haya ni jukwaa muhimu la kuonesha kwa vitendo namna Serikali inavyotekeleza mipango yake ya maendeleo kwenye sekta hizi muhimu,” amesema.

Akitolea mfano, Mhe. Kunenge amesema uzinduzi wa Reli ya Kisasa ya Mizigo (SGR) uliofanywa na Rais Dkt. Samia Julai 31, 2025 kule Kwala, mkoani Pwani, ni fursa muhimu kwa wakulima kwani utarahisisha usafirishaji wa mazao kwa haraka na kwa gharama nafuu, hivyo kuchochea uchumi wa kilimo.

Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Mashariki yanajumuisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga, na yanaendelea chini ya kaulimbiu:
“Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *