Na Mwandishi Wetu, Bariadi
NAIBU Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Bariadi, Injinia Kundo Mathew, amepitishwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyoketi hivi karibuni jijini Dodoma.
Kundo ametajwa kuwa mmoja wa watiania wanne wa jimbo hilo ambao majina yao yatapelekwa kupigiwa kura za maoni kwa ajili ya kupata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho tawala kwenye uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa Bariadi Mjini wamesema, wamefurahishwa na maamuzi hayo ya vikao vya CCM kwa kurudisha jina la mbunge wao ambaye wamekiri amewatendea haki kwa kipindi alichokaa bungeni na wameridhishwa na utendaji wake.
Walisema, wanachosubiri ni michakato ya ndani ya CCM ikamilike huku wakiwa na matumaini makubwa ya jina la mbunge huyo kurudishwa ili wampigie kura za kishindo arudi bungeni kuwatumikia.
Wananchi hao waliwasihi wajumbe wanaohusika kupitisha wagombea kutofanya makosa na kuhakikisha wanampitisha Mhandisi Kundo kuwa mgombea ili aendelee na kazi nzuri aliyoianza ya kuwaletea maendeleo kwenye jimbo lao.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, miradi mbalimbali imetekelezwa kwa mafanikio kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Kata ya Mhango, ambayo miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 6.4 imetekelezwa dani ya miaka mitano.
Akizungumza kwenye moja ya mikutano ya kuelezea utekelezaji wa ilani, Mhandisi Kundo alisema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi ya Maendeleo huku akiwataka wananchi kuendelea kuiamini na kwamba, ikifika Oktoba wamchague Rais Samia pamoja na viongozi wengine wa CCM.
“Tulikabidhiwa Ilani ya CCM, tumekuja kuwapa taarifa tulichokifanya kwa miaka mitano. Kata hii imepokea Shilingi Bilioni 6.4 Kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” alisema.