
MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema vijana wengi wanaojiunga na mafunzo ya Jeshi hilo hufika kwenye makambi wakiwa na hofu kwa sababu hawajui watakachokutana nacho, lakini wanapofikia mwisho wa mafunzo hayo hujikuta wakitamani kuendelea kubaki kwenye makambi hayo.
Meja Jenerali Mabele
ameyasema hayo leo Mei 21, 2025 Jijini Dodoma, akiwa katika kikosi cha jeshi hilo cha Makutupora wakati wa mahojiano kwenye kipindi cha Jambo Tanzania cha Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC).
“Kwa kawaida binadamu huogopa kitu ambacho hakijui, mara nyingi unapokabili kitu ambacho hukijui kikoje huwa unapata hofu, lakini mimi nipende kuwatoa hofu mafunzo haya vijana wengi wanapofika hapa wapo wanaokuja na hofu lakini anapotoka hapa anatamani kuendelea kukaa hapa, anatamani kuendelea kukaa ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa sababu vipo vingi anajifunza ambavyo hakuvizoea kule nyumbani”, amesema.
“…Wanalala kwa utaratibu sio kwamba mtu aamue tu mimi nitalala saa saba mimi nitalala saa mbili hapana, kuna utaratibu wa kufanya kazi ratiba ipo, hii ni ratiba ya kulala hii ni ratiba ya kuamka na unapoamka tunataka tuone kitanda chako umekitandika vizuri ndipo utoke sio ukurupuke tu unaacha kitanda shuka umeliviringisha lipo pale juu ya kitanda hapana…”. amesema Mkuu huyo wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele.
Na Mwandishi Wetu