📌Ni kuhusu sakata la kiwanja namba 170A kipawa jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Mfanyabiashara mwenye asili ya Asia, Bw. Satesh Khumal anadaiwa kukahidi wito wa Mawaziri wawili wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu kupeleka Wizarani nyaraka halali za umiliki wa kiwanja namba 170A eneo la Kipawa, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Mawaziri hao ni Jerry Silaa na Deogratias Ndejembi wa sasa ambao kwa nyakati tofauti inadaiwa walimuita Mfanyabiashara huyo kupeleka nyaraka halali za umiliki wa kiwanja hicho ili kutatua mgogoro wa eneo hilo ambao umedumu kwa takribani miaka 14.

Taarifa ambazo mwandishi wa habari hii amezipata ni kwamba, Silaa na Ndejembi walifanya juhudi za makusudi kusuluhisha mgogoro wa eneo hilo ambalo ni mahususi kwa ajili ya viwanda (Industrial area).

Taarifa zinasema, eneo hilo lilikuwa miliki ya marehemu wawili, Asha Binti Mwinyikondo na Buna Binti Musa ambao ni ndugu wa kuzaliwa na walikuwa na hati ya Mkoloni na walianza kumiliki eneo husika hata kabla ya Uhuru wa Tanganyika 1961.

Inaelezwa, baadaye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chini ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ilichukua sehemu ya eneo hilo na Kujenga Reli ya Tazara.

Baada ya kufariki wamiliki hao wa eneo husika, ndipo Bi. Mwanaidi Alawi akachaguliwa na familia kuwa msimamizi wa mirathi wa eneo hilo la marehemu hao wawili ambao ni shangazi zake, ambapo ndugu zake wamemthibitishia mwadishi kwamba Bi. Mwanaidi Alawi alifariki dunia mwaka 2016.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu, Msimamizi wa mirathi ya marehemu Bi. Mwanaidi Alawi, Ndugu Mbwana Alawi alisema kwamba mgogoro wa eneo husika ulianza kufukuta rasmi baada ya kifo cha shangazi yake Bi. Mwanaidi ambaye alifariki dunia 2016 na kulazimika kukimbilia Wizarani ili kupata msaada.

“Kwa ujumla kampuni hii ya Petro Fuel imekaidi maelekezo ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratias Ndejembi ya kukabidhi kiwanja namba 170A eneo la Kipawa , Wilaya ya Ilala kwangu kwa sababu tayari Waziri amenipatia hati namba 149078,”

Aliongeza, “huyu mmiliki wa Petro Fuel aliitwa mara kadhaaa toka mwezi wa tano mwaka jana hadi tarehe 3 mwezi machi mwaka jana na kutofika kwake kulitolewa maamuzi ya mimi kupewa hati nyingine na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Na hati hiyo nilipewa baada ya kutoka tangazo kwenye gazeti kwa siku 30 zikapita bila pingamizi lolote na wizara kutoa hati halali kwangu pamoja na Waziri Ndejembi kutoa maelekezo ya kampuni ya Petro Fuel kuondoa walinzi wake kwenye kiwanja husika lakini bado kampuni hii imekaidi maagizo hayo ya Waziri,” alisema kwa masikitiko makubwa.

Alifafanua zaidi kwamba, baada ya maamuzi hayo ya Waziri, Bw. Mbwana Alawi akiwa na mjomba wake mwingine walitembelea eneo hilo lakini cha kushangaza walikamatwa na Polisi kutoka kituo cha Buguruni na kuwekwa ndani na kufunguliwa kesi ya kutishia kuua kwa kutumia silaha na mpaka leo kesi hiyo bado ipo kituoni.

Msimamizi huyo wa mirathi wa eneo hilo, aliongeza kwamba nyakati tofauti aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa alimtaka mmiliki wa kampuni ya Petro Fuel Bw. Satesh Khumal kufika wizarani ili kuwasilisha nyaraka muhimu za umiliki wa kiwanja hicho, lakini mara kadhaa alishindwa kufanya hivyo na kutuma wasaidizi wake ambao waliwasilisha nyaraka na saini zilizoghushiwa.

Kwa Mujibu wa Bw. Alawi, Petro Fuel kupitia msaidizi wa Tajiri huyo mwenye asilia ya kiasia Bi. Mashamsham Dorice wanadai kwamba mwaka 2013 walimpa Mwanaidi Alawi kiasi cha Tsh 20 milioni.

“Ni kweli shangazi yangu alichukua fedha taslimu hizo na hata mwaka 2015 walimpa kiasi cha Tsh 30 millioni marehemu shangazi yangu, Bi. Mwanaidi Alawi na aliweka saini ya dole gumba maana alikuwa hajui kusoma na kuandika,” alifafanua Alawi.

“Kwenye haya malipo ya awali ni kweli shangazi alipokea ila alisema fedha nyingine inayobaki kiasi cha Tsh 610 milioni kiwekwe kwenye benki ambapo kampuni hiyo ya Petro Fuel haijafanya hivyo mpaka umauti unamfika,” alisema Alawi.

Alawi alisema, nyaraka walizoleta kampuni ya Petro Fuel Wizarani ni kwamba uhamisho wa umiliki wa eneo (Valuation Transfer) malipo yanaonyesha na saini yalifanyika 2018 na 2019 ambapo tayari shangazi yake mwanaidi Alawi alikuwa ameshafariki.

“Jambo la kushangaza ni kwamba nyaraka zao za mwaka 2018 na 2019 ya uhamisho wa umiliki kutoka kwa Mwanaidi Alawi kwenda Petro Fuel ilifanyika wakati shangazi alikuwa ameshafariki na saini yake wakati alikuwa hajui kusoma wala kuandika inashangaza kwa kweli,” alisema kwa uchungu Alawi na kuongeza kuwa, Jerry Silaa akiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi suala hilo lilifika mezani kwake na likaanza kushughulikiwa na maafisa wa Wizara akiwemo Kamishina wa Ardhi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika moja ya barua ambayo mwandishi wa habari hizi amezipata kutoka kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ya 24/05/2024 kwenda kwa kampuni ya Petro Fuel iliyoitaka kampuni hiyo kuwasilisha nyaraka za umiliki wa kiwanja tajwa iliyosainiwa, barua hiyo ilisainiwa na Bw. Burton Rutta kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.

“Ila cha kushangaza mara kadhaa alikuwa akiitwa na kuandikiwa barua rasmi za serikali ikimtaka aweze kufika kuleta nyaraka za umiliki wa kiwanja, hafiki isipokuwa alifika mara moja na msaidizi wake , Bi. Mashamsham Dorice na alileta nyaraka ambazo zinasaini ya Bi. Mwanaidi Alawi, wakati shangazi yangu alikuwa hajui kusoma na kuandika na kuweka saini alikuwa anatumia dole gumba,” alisema Alawi.

Mwandishi wa Habari hii alifanya juhudi za kumtafuta Waziri mwenye dhamana ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Bw.Deogratias Ndejembi ili kujua kuhusu sakata hili ambalo inadaiwa lilifika mezani kwake na alilitolea maamuzi.

Alipotafutwa kwa njia ya simu ya kiganjani kupitia (whattsap) Waziri Ndejembi aliomba atumiwe maelezo kuhusu eneo hilo la mgogoro na alipotumia na mwandishi akasema apewe muda akirudi ofisini ataangalia mpaka tunakwenda hewani bado hatujapata majawabu ya Waziri kama ni kweli alitoa hati mpya kwa Bw. Mbwana Alawi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Wakati huo huo , Mwandishi wa Habari hii pia alifanya juhudi za kumtafuta Bi. Mashamsham Dorice wa kampuni ya Petro Fuel ili kupata maelezo na ufafanuzi kwa upande wao ili alisema kwamba yupo nje ya ofisi akirudi ataweza kuwa na ufafanuzi.

Pamoja na juhudi za kumpigia simu yake ya kiganjani na kutuma ujumbe kupitia njia ya whattsap na maswali kadhaa, Bi. Dorice alishindwa kutoa ufafanuzi au kujibu sakata la kiwanja hicho mpaka tunakwenda mitamboni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *