NA MWANDISHI WETU

Kuna maswali mengi wananchi wa jiji la Dar es Salaam, hususani wale wanapendelea kufika kati kati ya jiji hilo, wanajiuliza kwa nini polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wanakamata watu wanapumzika kwenye bustani maarufu iliyoko katikati ya jiji hilo maeneo ya Stesheni mtaa wa Samora maarufu kama Kaburi moja.

Sasa hivi imeshakuwa ni kawaida polisi hususani wa Kituo cha Kati(Central) kuwakamata watu mbalimbali wakiwa wamepumzika katika bustani hiyo barabara ya Samora maarufu kama’ Kaburi moja’.

Mwaka 2017 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, alifanya juhudi kubwa ya kuboresha bustani hiyo ili wananchi wapumzike nyakati za mchana baada ya kazi ngumu au wakati wakisubiri kuingia katika harakati zao za mahangaiko.

Mheshimiwa Makonda alizindua bustani hiyo na kuweka jiwe la msingi, aliagiza watumiaji wa bustani hiyo kuitunza na bustani hiyo na kweli inatunzwa mpaka leo.

Ukimuondoa Makonda ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,bado aliyemfuatia kuongoza Dar es Salaam Mheshimiwa Abubakar Kunenge, aliendeleza bustani hiyo na kuwafanya wakazi wa eneo hilo kujivunia bustani yao inayomilikiwa na jiji.

Mheshimiwa Kunenge naye akahamishiwa Mkoa wa Pwani na kumwachia kijiti Mheshimiwa Albert Chalamila, ambaye bado yupo mpaka Leo. Naye kaendeleza bustani hiyo kwa kuwaongezea viti wananchi wake baada ya kubaini vilivyokuwepo ni vichache sana kulinganisha na watu wanaokuja kupumzika bustanini hapo.

Katika hali ya kawaida serikali iliingia gharama kubwa ili kujali watu wake lakini hivi sasa polisi wanawasumbua sana watumiaji wa bustani hiyo kwa kuwakamata kwa kosa la uzembe na uzururaji makosa ambayo yalikuwepo miaka ya themanini wakati operesheni nguvu kazi.

Wanacholalamikia wananchi ni jinsi polisi wanavyokamata watu hovyo, bila kuchagua bodaboda, wastaafu wanaofuatilia viinua mgogo vyao na hata wale ambao wanasubiria muda ufike wa kuona wagonjwa wao waliolazwa kwenye hospitali zilizo karibu na bustani hii mfano Hindu Mandalai, Aga khan na Burhan.

Hata wakijieleza hawasikilizwi na kuondoka nao lakini baadaye wanarudi na wengine wanafuatwa na ndugu zao ambao wanaenda kuongea na polisi kwa hekima.

Inasikitisha wakati mwingine hata vichaa kabisa wanakamatwa tunawaomba polisi kama wanatafuta wahalifu washirikiane na wananchi ili kutimiza lengo la usalama wa raia na mali zake jambo ambalo linatakiwa sana katika zana ya ulinzi shirikishi.

Morningstar Post inaendelea kumtafuta Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Mlilo kuzungumzia suala hili.

Mungu ibariki Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *