WANANCHI wa kijiji cha Kanutwa, Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya, wamelalamikia vitendo vya unyanyasaji wanavyodai kufanyiwa na wakulima wakubwa kwa kuwatumia baadhi ya askari polisi Wilayani humo.

Akizungumza na MorningStar Post kwa niaba ya wananchi wa kijiji hicho, Lawrance Mwampelwa alisema, katika kipindi hiki cha kuandaa mashamba, wanashindwa kufanya hivyo kwasababu wanazuiwa na polisi kuingia kwenye mashamba yao.

Mwampelwa alisema, baadhi ya wakulima hao wanawatumia askari wa ngazi za chini na vijana wa kihuni kuwanyanyasa na wanahisi huenda wanapewa fedha kwa ajili ya kuwafanyia vitendo hivyo ikiwemo kuwapiga, kuwapora majembe, simu na fedha ili kuwatisha wasiendeleze mashamba yao.

Taarifa zaidi kutoka kijijini hapo zinadai kwamba, sababu ya wafanyabiashara hao kuwazuia kuingia kwenye mashamba yao ni kutaka wayaache ili wao wayachukue kwa nguvu.

“Huu ni msimu wa kilimo na tunatakiwa kuandaa mashamba, lakini kuna watu wenye nguvu ya fedha wanatumia uwezo wao kutuzuia kuingia mashambani ili tukiyaacha wayapore, hii sio haki kabisa. Tunaiomba Serikali yetu sikivu hususani kwa Mkuu wa Wilaya yetu atusaidie ili tuendelee na shughuli zetu za kilimo ambazo ndio zinatufanya tuishi na familia zetu,” alisema mwananchi mwingine ambaye hakupenda kutaja jina lake.

Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Maulid Surumbu kwa njia ya simu, alikiri kupata taarifa hizo na kusema, Jeshi la Polisi linaendelea kufanyia kazi malalamiko hayo ya wananchi wa kijiji cha Kanutwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *