WAKULIMA na wafugaji wa Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya, wamemuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza sakata la maeneo yao kuchukuliwa na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (Ruaha National Park).
Walisema, hivi karibuni walimsikia Rais Samia wakati akizungumza na wazee wa kimila wa jamii ya kabila la wamasai, Laigwanan mkoani Arusha, akiahidi kuunda tume mbili kwa ajili ya kuchunguza zoezi la kuwahamisha wakazi wa eneo hilo kutoka wilaya ya Ngorongoro kwenda wilaya ya Msomera, Mkoani Tanga, jambo ambalo limewapa faraja na kuamini nao wanaweza kufikiwa.
Kwenye mkutano huo, Rais Samia alisema tume ya kwanza ni ile itakayoangalia masuala ya ardhi katika eneo hilo na tume ya pili itakuwa huru, itakayoangalia suala zima la kuhama Ngorongoro, itakayohusisha watu wachache watakaofanya utafiti na kutoa majibu.
Wananchi hao wa Mbarali wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema, suala la kuhamishwa kwao linapotoshwa na limegubikwa na mizengwe mingi, hivyo kunahitajika uchunguzi wa kina ili kulipatia ufumbuzi, kwani limedumu kwa miaka mingi na linasababisha athari kubwa kwa uchumi wao.
Kwa mujibu wa barua yao ya Oktoba 10, 2024, yenye KUMB. NA. MBR/WF/B.01/010/024 wananchi hao walisema, ardhi yao ilichukuliwa mwaka 2007 na 2008 wakati wa upanuzi wa mpaka wa hifadhi hiyo, ambapo ilihusisha Kata ya Msangaji na vijiji vyote, na baadhi ya vijiji vya Ikiga Kata ya Madibira.
Aidha, upanuzi huo ulihusisha pia vitongoji vya Itagavanu, Kapunga, Kata ya Igava na likaongezwa eneo la Ihefu, ambapo wananchi wa vijiji hivyo walilipwa fidia.
“Uwekaji wa ‘beacon’ ulitushangaza wananchi wa Mbarali, badala ya kuweka walipohamisha watu, zikawekwa kwenye maeneo ya makazi na mashamba ya watu ambao hawakuhusika na uhamisho” ilisema barua hiyo.
Iliendelea “viongozi wa TANAPA walipoulizwa kwanini wanaweka ‘beacon’ kusikohusika? Walijibu kuwa, ni bahati mbaya ndege ilipokuwa inaweka alama za mipaka ilikosea, ingawa hadi leo hawajarekebisha kasoro hiyo. Hiki ndicho kiini cha mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Wilaya ya Mbarali na TANAPA.”
Wananchi hao walidai, wataalamu ndio chanzo cha mgogoro huo, kwani makosa hayo waliyafanya kwa makusudi kwa msukumo wa baadhi ya watu wanaotaka eneo hilo la kilimo na ufugaji la wananchi wa Mbarali.
“Hata aletewe kiongozi mzuri, wasipoondolewa Afisa Ardhi wa Wilaya, mwanasheria na Afisa Mipango wa Wilaya, bado hawa wataendelea kupotosha ukweli kwasababu inaonekana ipo namna kati yao na mabepari kuendelea kuandika taarifa za uongo kwa ngazi za juu Serikalini” ilisema barua hiyo.
Wananchi hao kupitia barua hiyo ambayo mwandishi wa habari hizi anayo, walisema miongoni mwa sababu zinatumiwa na watendaji hao ni ardhi oevu, vyanzo vya maji, mazingira “hali halisi ya Mbarali hakuna vyanzo vya maji, ila ni mapito ya maji toka milima ya Makete, hivyo suala la mazingira lina sheria yake ya mita 60 toka mto hakuna mwananchi anayeweza kupinga.
Walisema, Oktoba 25, 2022 aliyekuwa Waziri wa Ardhi Angelina Mabula kwenye mkutano wa hadhara akiwa na Kamati ya bunge, aliagiza wakulima na wafugaji waondoke mashambani na kwenye maeneo wanayoishi ili kupisha upanuzi wa Hifadhi ya Ruaha, wakati tayari kulikuwa na agizo la Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Mrisho Kikwete la kutoongeza eneo kwa ajili ya kupanua hifadhi hiyo.
“Rais Kikwete alipoondoka madarakani, mgogoro uliibuka upya. Mwaka 2015, Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi, alisema hatakubali kuona wananchi wa Mbarali wananyang’anywa ardhi yao na yeyote atakayejihusisha na kuhamisha wananchi wa Mbarali, kama ni mtumishi wa Serikali basi utumishi wake utaishi hapo” iliendelea barua hiyo.
Hata hivyo, licha ya maagizo ya viongozi hao, bado wananchi hao wamezuiwa kuendelea na shughuli yoyote ndani ya maeneo hayo ambayo wanasema wanamiliki kihalali kwa miaka zaidi ya 30.
“Tunamuomba Rais alione hili ombi letu, atusaidie wananchi wa Mbarali waachiwe ardhi yao ambayo ndio ajira yao katika kuendesha maisha yao na makazi” walisema.
“Wananchi wa Mbarali tuna imani na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa anawapenda watanzania wote na kamwe hawezi kuruhusu ubaguzi kwa wananchi wake,” waliongeza.
Aidha, wamuomba Rais Samia kupitia watumishi wake waadilifu wafike Mbarali kwa ajili ya kuona ukweli huo ili wananchi wa maeneo hayo waruhusiwe kulima wakati wakisubiri maamuzi ya mahakama au Serikali, kwani wana mikopo ya kilimo kwenye benki mbalimbali na wengine dhamana zao zimeanza kuuzwa na benki baada ya kushindwa kulipa mikopo hiyo.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa, kuchukuliwa kwa eneo kutaathiri soko la mpunga kwani robo tatu ya mashamba ya kilimo cha mpunga Wilayani Mbarali.
Pia, kuna viwanda zaidi ya 70 vya kukoboa zao la mpunga, hivyo vitakosa malighafi “Serikali itaingia hasara kwa kuagiza mchele kutoka nje ya nchi wakati Mbarali inazalisha tani nyingi za mchele na ushahidi ni gari kubwa zaidi ya 15 kila siku zinasafirisha mchele kutoka Mbarali na kulisha mikoa mingi ya Tanzania na nje ya nchi.”
Vile vile, iwapo ardhi hiyo itatwaliwa na Serikali, wananchi zaidi ya 100,000 (Laki moja) watapoteza ajira “kuna nyaraka kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya zina maelekezo ya kibaguzi kuwa, hakuna ruhusa ya kulima maeneo haya, ukifuatilia anasema ni maagizo kutoka juu. Huku ni kumchafua Mh. Rais.”
Mwandishi wa habari hizi hakufanikiwa kuwapata viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ili kujua ni lini watarekebisha mipaka ya eneo hilo na kumaliza mgogoro huo, hata hivyo jitihada zinaendelea.