Na Mwandishi Wetu

Hivi karibuni serikali ya Tanzania na Kampuni ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC), zilisaini makubaliano ya ujenzi wa Daraja la mita 390 kwenye eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam.

Mkataba wa ujenzi wa daraja hilo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na barabara za maungio zenye urefu wa mita 700 katika barabara ya Fire – Ubungo kwa gharama ya Tsh 97.1 billioni ambapo kazi ya ujenzi itatekelezwa kwa miezi 24.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ujenzi, imesema Wakala wa Barabara wa Nchini (TANROADs), imetia saini makubaliano hayo na kampuni ya China kwa niaba ya serikali, huku hafla ya utiaji saini ikishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi Bw. Innocent Bashungwa.

Wakati hayo yakifanyika, kumbukumbu zinaonyesha kwamba kampuni hiyo iliyopewa tenda kutoka China , iliwahi kumuweka matatani aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA), Bw. Ephraim Mgawe kuhusu matumizi mabaya ya Madaraka.

Mkurugenzi huyo Mtendaji wa zamani wa TPA, Ephraim Mgawe na aliyekuwa Naibu wake, Hamad Koshuma walikuwa na kesi ya kujibu ya matumizi mabaya ya madaraka.

Mgawe na mwenzake walipanda kizimbani katika kesi ya aina yake 2016 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kutoa zabuni kwa kampuni ya China ya Communication Construction Company Limited (CCCCL) kwa ajili ya ujenzi wa magati katika Bandari ya Dar es Salaam.

Aliyekuwa, Hakimu Mkazi Cyprian Mkeha ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama ya Biashara aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alisema kwamba ameridhika kuwa upande wa mashtaka umeweza kujenga hoja dhidi ya washtakiwa hao na kuwa wana kesi ya kujibu.

“Baada ya kupitia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka pamoja na vielelezo, nimeridhika kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu, hivyo wanatakiwa kutoa utetezi wao,” alisema hakimu Mkeha.

Mgawe na Koshuma walidaiwa kula njama na kutoa zabuni tata kwa kampuni hiyo kwa ajili ya kujenga maghati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa gharama ya Dola 600 milioni (Sh1.3 trilioni) kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kusaini mkataba wa kibiashara na kampuni hiyo bila zabuni shindanishi kinyume cha sheria hiyo ya manunuzi ya umma.

Juhudi za kuwatafuta mamlaka husika juu ya uwezo , historia , uwajibikaji pamoja na uaminifu kampuni hiyo husika kuhusu kutekeleza mradi wa ujenzi wa daraja la jangwani na historia ya kampuni zinaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *