
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Ndg. Rajabu Abdulrahman Abdallah (Kushoto)
Na Mdoe Kiligo, TANGA
KAMATI ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Septemba 26, 2024, imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, ikiwa ni matakwa ya Katiba ya chama hicho katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya chama.
Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Ndg. Rajabu Abdulrahman Abdallah, ilitembelea jumla ya miradi nane iliyo katika sekta za elimu, afya, barabara na miundombinu ya wafanyabiashara, ambapo kamati ilipokea taarifa ya utekelezaji na kujionea uhalisia wa mradi.
Kamati ilianza kwa kutembelea mradi wa jengo la Machinga Kange, Ujenzi wa wodi katika hospital ya Wilaya iliyopo Masiwani, ujenzi wa nyumba ya mtumishi kituo cha afya Tongoni, jengo la utawala na maabara katika Shule ya Sekondari Kiomoni, na ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Mafuriko.
Kamati pia ilitembelea ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi katika shule ya msingi Mabokweni, ujenzi wa madarasa shule ya msingi Kiruku na ujenzi wa barabara kiwango cha lami katika kata ya Mabawa.
Mwenyekiti Rajabu amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Chama na Serikali katika Wilaya ya Tanga, katika kuhakikisha miradi inakamilika. Amesema wakazi wa Tanga wanahitaji maendeleo na kwamba Tanga sio sehemu ya kujifichia wezi wa mali za umma, na wote watakao bainika kufanya ubadhirifu, sheria itachukua mkondo wake.
Amewataka wazazi kusimamia elimu ya watoto, kwani Serikali imeboresha miundombinu na mazingira ya kujifunza na kufundishia, huku ikifuta ada kwa wanafunzi elimu ya awali hadi kidato cha sita. Hivyo, hakuna sababu ya watoto kutokufanya vizuri katika masomo yao.
Ziara hiyo pia ilimshirikisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Japhari Kubecha, Mstahiki Meya wa Jiji Mhe. Abdulrahman Shiloow, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Mhandisi Juma Hamsini, Katibu Tawala Ndg. Dalmia Mikaya, na viongozi wengine.