
Baadhi ya Wanawake wakipata maelekezo katika Banda la Bodi ya Mkomge Tanzania (TSB) kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (sabasaba) jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu, TSB
MAONESHO ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yamehitimishwa katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo wanawake wengi wamejitokeza kutaka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo cha Mkonge kulinganisha na wanaume.
Afisa Kilimo wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Emmanuel Lutego amesema hayo kwenye banda la Bodi ambayo imeshiriki maonesho hayo tangu siku ya kwanza Juni 28, mwaka huu.
Amesema katika wanawake hao, wapo wenye mashamba hadi ya ekari 100 ambao wametaka kupata elimu kuhusu uwekezaji wa kilimo hicho.
“Maonesho ya mwaka huu ni tofauti kabisa na ya miaka mingine iliyopita. Wanawake wamekuwa na mwamko mkubwa wa kutaka kujifunza kuhusu zao la Mkonge kwenye banda letu.
“Wako wengine ambao wametoa ushuhuda kuhusu mafanikio waliyopata kuhusu kilimo hicho katika mashamba yao wanayolima hivyo kutaka kupata ushauri wa kitaalamu Zaidi,” amesema Lutego.
Pamoja na mambo mengine, amesema kuna wanawake ambao wamesema wameshandaa mashamba na wanataka kuingia kwenye sekta ya Mkonge ili kuanza kulima na kupata faida huku wengi wao wakiiomba serikali kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya usindikaji ikiwamo mashine za kuchakata Mkonge.
“Kama nchi kuona wanawake wanaingia sekta ya kilimo hasa Mkonge ni hatua kubwa kwa taifa. Tunachoahidi kama TSB ni kuwapa ushirikiano wa kutosha ili walime kwa faida kubwa,” amesema Lutego.