Waziiri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda

Na Mdoe Kiligo, MeCAP

SERIKALI ya Tanzania imesema itaendelea kuboresha elimu ya ufundi ili kuwapatia vijana ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa na kuajirika.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda Julai 9, 2024, jijini Dar es Salaam alipokutana na uongozi wa Taasisi ya Mfalme wa Uingereza ya King’s Trust International.

Prof. Mkenda amesema mazungumzo na Taasisi hiyo yapo kwenye hatua nzuri, huku lengo kuu la taasisi hiyo likiwa ni kuvijengea uwezo vyuo vya ufundi hapa nchini ili viweze kuzalisha vijana wenye ujuzi kamili unaoendana na teknolojia ya kisasa katika fani zao.

“Tumeiomba taasisi ya King’s Trust International, mbali na kusaidia eneo la mafunzo ya lugha, watoe pia mafunzo ya ufundi stadi kwa vyuo viwili vya VETA na watusaidie eneo la ujuzi katika fani mbili, moja ikiwa ni Mekatroniki, yaani ujuzi wa kumwezesha kijana kutengenza magari ya kisasa yanayotumia umeme mwingi ama umeme peke yake na eneo la ushonaji wa nguo katika mitindo mbalimbali,” alisisitiza.

Alifahamisha pia utashi wa serikali kuwa na vyuo vya kuzalisha wataalamu wanaoendana na teknolojia ya kisasa na hata kuwa na vyuo ambavyo vitakuwa na kampuni za kuzalisha na kuuza bidhaa husika.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Vyuo wa NACTVET, Dkt. Amani Makota amesema ziara hiyo imekua ya manufaa makubwa katika kuangazia maeneo mengine ambayo Tanzania inaweza kufanya ushirikiano na Taasisi hiyo.

Dkt. Makota amesema maeneo lengwa yanategemewa kufanyiwa mabadiliko makubwa sana kwenye sekta ya ufundi ni katika kusaidia vijana kupata ujuzi kulingana na teknolojia za sasa.

“Baada ya ushirikiano huu tunategemea vijana wetu watakuwa na ujuzi na mbinu ambazo zinapatikana duniani kote,” alisema Dkt. Makota.

Aliongeza kuwa ni wazi sekta ya ufundi nchini itaenda kuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye sekta mbalimbali na kusisitiza kwamba huo ni mwanzo tu utakaokuwa na mwendelezo mzuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *