BBC, Nairobi
Kizazi kipya cha waandamanaji wachanga wa Kenya kimeibuka barabarani na kulazimisha serikali kubadilisha baadhi ya mapendekezo ya kodi ambayo hayakuwapendeza watu wengi nchini humo.
Kilichoanza kama hasira katika TikTok kuhusu mswada wenye utata wa fedha kimebadilika na kuwa uasi – bila kupangwa na vyama vya siasa.
Serikali ya Rais William Ruto imeweza kufanya kile ambacho vizazi vya wanasiasa katika taifa hilo la Afrika Mashariki vimeshindwa kufanya – kuunganisha idadi kubwa ya Wakenya bila kutumia ukabila au vyama .
Siku ya Jumanne, mamia ya waandamanaji ambao wanahisi Wakenya tayari wametozwa ushuru kupita kiasi bila ya kuwa na ufanisi unaooneysha jinsi kodi yao inavyotumika , walistahimili makali vitoa machozi na mapambanano na polisi kuandamana katika mji mkuu, Nairobi, na kusababisha shughuli katikati mwa jiji kuvurugwa.
Wakiwa na simu zao za mkononi, walipeperusha moja kwa moja makabiliano makali na maafisa wa polisi.
Maandamano hayo yaliyopewa jina la “kuchukua bunge” yaliratibiwa na kuhamasishwa kwenye mitandao ya kijamii tofauti na yale yaliyokuwa yakiongozwa na kufadhiliwa na wanasiasa.
Waandalizi waliwahimiza waandamanaji wenzao kuvaa nguo nyeusi, lakini wengine bado walijitokeza wakiwa wamevalia jeans zilizochanika na nywele maridadi.
Waandamanaji vijana, maarufu kama Gen Zs – kwa kurejelea neno linalotumiwa kwa ujumla kuwaelezea wale waliozaliwa mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 – walijitokeza kwa wingi, wakiapa kuhakikisha kwamba kutoridhika kwao hakuishii kwa alama ya reli tu au vibonzo vya kejeli mtandaoni.
“Sisi ni Gen Z, tuliweza kujipanga. Tunatumia TikTok kama kifaacha kuweza sio tu kuwahamaisha vijana kuja kuandamana bali kuwaelimisha ni kwa nini tunafanya hivyo,” mwandamanaji Zaha Indimuli aliwaambia waandishi wa habari.
Wengi wao walikuwa wakiandamana kwa mara ya kwanza na kutikisa mabango yenye maneno kama vile “Usilazimishe Ushuru” , huku wengine wakiimba: “Ruto lazima aondoke”.
“Niko hapa nikitumikia nchi ninayoipenda. Ni mara ya kwanza ninafanya hivi kwa sababu wazazi wangu ni wazee na hawawezi kufanya hivyo tena,” Ken Makilya, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 24, aliiambia BBC.