BBC

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amevunja baraza lake la mawaziri sita la vita, ikiwa ni wiki moja tu baada ya kuondoka kwa kiongozi wa upinzani Benny Gantz na mshirika wake Gadi Eisenkot.

Vyombo vya habari vya Israel vinaripoti kuwa masuala nyeti kuhusu vita na Hamas huko Gaza sasa yatajadiliwa na jukwaa dogo.

Bw.Netanyahu alikabiliwa na matakwa kutoka kwa mawaziri wa siasa kali za mrengo wa kulia katika muungano wake tawala kujiunga na baraza la mawaziri la vita, ambalo lingeweza kuzorotesha zaidi uhusiano na Marekani na washirika wengine wa kimataifa.

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) alisema kuwa, haitaathiri utaratibu wa kiitifaki.

Bw.Gantz na Bw Eisenkot walijiuzulu kutokana na uongozi wa waziri mkuu, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa mpango wa baada ya vita Gaza.

Wakuu hao wawili wa zamani wa kijeshi walikuwa wamejiunga na serikali ya umoja wa kitaifa na muungano wa mrengo wa kulia wa Bw Netanyahu siku baada ya kuanza kwa vita mwezi Oktoba.

“Baraza la mawaziri la vita lilikuwa katika makubaliano ya muungano na Gantz kwa ombi lake.

Mara tu Gantz alipoondoka, hakuna haja ya baraza la mawaziri tena,” Bw.Netanyahu aliwaambia mawaziri Jumapili, kulingana na Jerusalem Post.

Haaretz iliripoti kwamba baadhi ya masuala yaliyojadiliwa hapo awali na baraza la mawaziri la vita yatahamishwa kwa ajili ya kujadiliwa katika baraza la mawaziri la usalama, ambalo linajumuisha Mawaziri wa Usalama wa Kitaifa na Fedha wa mrengo mkali wa kulia, Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich.

Ilisema maamuzi nyeti yatashughulikiwa katika “jukwaa dogo la mashauriano”, ambalo lilitarajiwa kujumuisha Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, Waziri wa Masuala ya Mikakati Ron Dermer na mwenyekiti wa chama cha ultra-Orthodox Shas, Aryeh Deri, ambaye alikuwa mwangalizi katika baraza la mawaziri la vita.

Msemaji mkuu wa IDF, Daniel Hagari alisema Jumatatu kwamba hatua hiyo haitaleta athari.

“Wajumbe wa Baraza la Mawaziri wanabadilishwa na mbinu inabadilishwa. Tuna echelon, tunajua safu ya amri. Tunafanya kazi kulingana na mlolongo wa amri. Hii ni demokrasia,” aliwaambia waandishi wa habari.

Jeshi la Israel lilianzisha kampeni huko Gaza kuiangamiza Hamas kujibu shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takribani watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.

Zaidi ya watu 37,330 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *