Shule ya Msingi na Ufundi Mbezi iliyoko wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Mbezi na Ufundi , Manispaa ya Ubungo, Kata ya Mbezi , Daniel Machage amesema kwamba michango yote kwa ajili ya mitihani ya mihula na Moko inafanywa baada ya kikao cha wazazi kuridhia kama muongozo wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi unavyotaka kwa kuwa Shule za serikali ni mkombozi wa elimu hapa nchini, Morningstar blog inaripoti.
Akizungumza ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Bw Machage amesema kwamba kila mwezi wa Juni huwa anafanya kikao na wazazi shule hapo ili kupata maendeleo ya kitaaluma kwa maslahi mapana ya watoto wa kitanzania.
“Sio kweli kwamba mimi nakusanya michango kwa wanafunzi kupitia wazazi wao bila kufanya nao vikao ,hapana huwa tunakuwa na vikao hapa tena safari hii nataka mje (waandishi) kwenye kikao , na naweka na spika kubwa mpaka kule stendi ya Magufuli wanasikia hii yote ni kwa manufaa ya hawa wananchi na watoto wa hapa Mbezi,” alisema kwa msisitizo.
Aliongeza kwamba ni kweli fedha kutoka serikali zinakwenda katika Shule hiyo kupitia Tamisemi kiasi cha shilingi 1.2 milioni kila mwezi ila ni kwa ajili ya ukarabati wa shule , miundombinu , vifaa na mambo ya michezo ikiwa ni pamoja na gharama zingine lakini kiasi hicho hakitoshi, na akasisitiza kwamba hawezi kukusanya fedha bila idhini ya wazazi , Mkurugenzi na kibali cha Mkuu wa Wilaya.
“Katika hiyo fedha 1.2 millioni utoe asilimia mbili ili uweze kugharamia mitihani ya mihula, moko na ya kata kwa wanafunzi wasipoungua 2,532 na darasa la saba pekee ni wanafunzi 291 hii (capitation) ya serikali haiwezi kutosha ndugu zangu,” alisisitiza.
Aliendelea kusema kwa kibali cha Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ingawa hakutoa maandishi ila yatakuja, madarasa ya mitihani kila wiki wanaweza kuchangia 1,500 na kwa madarasa ambayo hayana mitihani kila mwezi 1,000.
“Sasa sie hapa tunajibana bana kwa fedha ya madarasa ambao hawana mitihani tunakusanya kila mwezi tunagharamia mitihani ya kata hapa Shule ya Mbezi mitihani ya Kata hatukusanyi michango kutoka kwa wazazi,’ alisema kwa kujiamini.
Aliendelea kusema kwamba shule za serikali ni mkombozi kwa watanzania wengi hapa nchini kwa sababu watu wanapata nafasi ya kusomesha Watoto wao kwa gharama ndogo na wanapata elimu nzuri.
Awali blog hii ilimtafuta mwalimu huyo mkuu kutoa ufafanuzi wa tuhuma mbalimbali ikiwemo ya kukusanya michango kwa wanafunzi, kutumia lugha zisizo na staha kwa walimu na mahusiano mabaya na wenzake.
Akifafanua juu ya tuhuma hizo alisema kwamba sio kweli kwamba yeye anatumia lugha mbaya, bali anachofanya ni kusimamia kanuni, sheria na taratibu za serikali katika kuhakikisha taaluma inapanda shuleni hapo.
“Kama mimi ningekuwa na mahusiano mabaya na walimu wangu nisingeweza kupandisha kiwango cha ufaulu cha shule hii kwa sababu ufaulu unapanda kwa sasa shule hii ni ya 20 katia 80 katika wilaya ya Ubungo tunakwenda vizuri kwa kweli”, amesema.
Kwa Upande wake, Afisa Elimu wa Wilaya ya Ubungo, Bw. Nyoni amesema kwamba michango yote inayokusanywa shule lazima kuwa na vikao kati ya wazazi na uongozi wa shule na wazazi wanarishia kuchangia gharama za elimu hapa nchini.
“Sikia ndugu yangu fedha za serikali zinakwenda kila mwezi ila pale ambapo hapakutosha wanaweza kukusanya michango kama waraka wa serikali unanyosema na kibali kinatoka kwa Mkuu wa Wilaya (DC) na si vinginevyo,” alisisitiza Bw Nyoni
Bw Nyoni aliongeza kwamba taratibu zote za serikali zinafuatwa na sio kweli kwamba mkuu wa shule ya Mbezi anafanya kwa matakwa yake, ila kama kuna tofauti ameahidi kufuatilia.
Kwa Upande Mratibu wa Elimu Kata ya Mbezi, Bi Massawe amesema kwamba upande hajawahi kupata malalamiko hayo ya ukusanyaji wa michango ua mitihani shuleni hapo kama yapo anafuatilia.
Awali kulikuwa na tuhuma dhidi ya Mwalimu huyo Mkuu kwamba anafanya unyanyasaji kwa walimu , kukusanya michango bila vikao na wazazi na kuendesha shule kinyume na matakwa ya serikali.
Taarifa za awali zilidai kwamba Mwalimu Mkuu huyo ni mbabe , ana kiburi , anatoa lugha zisizo na staha kwa walimu wa kike na kufanya matendo ambayo ni kinyume cha maadili kwa viongozi wa umma, tuhuma ambazo amezikana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *