Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya wawekezaji mbalimbali kutoka nje ya nchi, wamedaiwa kutumia majina ambayo sio yao katika kuendesha shughuli zao hapa nchini.

Uchunguzi usio na mashaka wa mtandao huu unabainisha kwamba baadhi ya wawekezaji hao, kwa sababu ambazo hazijafahamika wazi hawataki kutumia majina yao sahihi katika baadhi ya shughuli wanazofanya jambo ambalo linatia mashaka.

Mtandao huu umebaini kwamba baadhi ya wawekezaji hao wamenunua baadhi ya kampuni zilizokuwa zinamilikiwa na Watanzania huku wakificha uwekezaji wao kwa kutumia majina ya wabia wao hapa nchini.

Mmoja wa mifano ambayo Mtandao huu imebaini ni raia mmoja wa China aitwaye Tom anayedaiwa kuwa na hisa katika kampuni ya Intertz Logistics ya Jijini Dar es Salaam ambaye amekuwa akitumia jina la mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo, Doreen Barongo.

Alipoulizwa kwanini hataki kutumia jina lake ikiwa ni pamoja na kwenye usajili wa simu, Mchina huyo alikataa kutaja jina lake analotumia kwenye hati yake ya kusafiria.

Tom anadaiwa kuwa amekuwa akitumia jina la Doreen Barongo katika usajili wake wa simu tangu awasili hapa nchini jambo ambalo ni kinyume cha Sheria kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano hapa nchini (TCRA).

Mtandao huu unaendelea na uchunguzi wake kuhusu tuhuma za baadhi ya wawekezaji hao hapa nchini kuficha majina yao kwenye miamala na shughuli mbalimbali wanazofanya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *