Na Waandishi Wetu

BAADHI ya Wafanyakazi katika kampuni ya kigeni ya Sinohydro Corporation inayojenga miradi mikubwa ya barabara jijini Dar es Salaam wameitaka serikali kumlazimisha mwajiri wao huyo kufuata Sheria za Kazi.

Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wafanyakazi hao wamesema wamekuwa wakifanya kazi siku zote 7 za wiki bila kupumzika na hawalipwi saa za ziada.

Wamesema katika kampuni hiyo kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za kazi, lakini viongozi wa kampuni hiyo kutoka nchini China wanaonekana kama wako juu ya sheria hizo na wamefumbiwa macho.

“Hizi kazi za ujenzi wa barabara kama mnavyoona ni kazi ngumu, sisi hapa tunafanya kazi siku zote. Hatuna sikukuu, hatuna Jumamosi wala Jumapili na tunaingia kazini kuanzia saa 1 asubuhi hadi saa 12 jioni. Ukiumwa wanakukata pesa”, amesema mmoja wao.

Mfanyakazi mwingine amesema pamoja na kwamba wanafanyakazi kwa mkataba wa mwaka mmoja, lakini haki nyingi zinakiukwa na hawana pa kusemea.

“Wakati huu wa mvua kwa mfano, tunafanya kazi mpaka saa 6 au saa 7 mchana kama mvua zimekuwa nyingi, lakini tunakatwa saa ambazo zimebaki. Sasa mbona tukifanya kazi saa 12 hawatupi fedha za siku nzima?”, amehoji.

Mfanyakazi mwingine amesema wanaiomba serikali, pamoja na umuhimu wa kutakiwa kumalizika barabara za mwendokasi kwa wakati Jijini Dar es Salaam, lakini pia wafanyakazi wapewe muda wa kupumzika na wapimwe afya zao, ili waweze kujenga barabara bora.

Mwezi Februari mwaka 2021, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke Godwin Gondwe aliikemea kampuni hiyo kwa kukiuka Sheria mbalimbali.

Gondwe aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inafanya kazi hiyo kwa thamani halisi ya fedha na kuheshimu taratibu za nchi.

Maofisa wa Kampuni hiyo wamefanya mahojiano na Waandishi wa Habari, na kujitetea kuhusiana na tuhuma hizo, majibu ambayo yatawekwa hadharani pamoja na yale ya taasisi zinazosimamia Sheria za Wafanyakazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *