
WATUMISHI wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo Stadi (NACTVET) jana waliungana na watumishi wengine ulimwenguni kusherehekea Siku ya wafanyakazi duniani.
Jana ilikuwa ni Mei Mosi na mwaka huu wa 2024, maadhimisho hayo kitaifa yalifanyika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Kaluta Jijini Arusha ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango akimwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Wakiwa wamevaa mavazi ya kupendeza watumishi hao walikuwa miongoni mwa watumishi wa idara na taasisi za umma waliong’ara zaidi katika maadhimisho hayo.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa wafanyakazi nchini kuendelea kutekeleza majukumu kwa bidii, maarifa, uadilifu kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele kwa kuongeza tija katika utendaji kazi.
Lakini pia amevisihi vyama vya wafanyakazi kushirikiana na Serikali na Waajiri kuhakikisha tija inaongezwa kwenye maeneo ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe.
Aidha amewaasa wafanyakazi kuwa mstari wa mbele katika kudai risiti kila wanaponunua bidhaa na kuhakikisha risiti wanazopewa zimeandikwa gharama halisi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato zaidi na kupelekea wigo mpana zaidi wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa yamehuduhuriwa pia na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko, Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Deogratius Ndejembi.
Wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Dkt. Moses Kusiluka, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) Tumaini Nyamhokya, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi John Mongela, Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, Mahakama, Vyama vya Wafanyakazi pamoja na wafanyakazi sekta binafsi na serikali.