
Na Paul Wakanay
WANANCHI wa Kijiji cha Kazole, Kata ya Vikindu mkoani Pwani wamemwalika kwenye Kijiji hicho, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amosi Gabriel Makalla.
Mwaliko huo ni kutokana na kile walichosema kwamba wamechoshwa na manyanyaso wanayopata kupitia baadhi ya wanasiasa kwenye kata na wilaya hiyo ya kumkumbatia mwekezaji mmoja anayewaonea.
Wakiongea na baadhi ya waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho, wananchi hao wamesema kwamba aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Dkt John Magufuli alikuwa amemaliza mgogoro baina yao na mwekezaji mmoja katika kijiji hicho kwa kuamuru kwamba wakulima waachwe wafanya shughuli zao bila kunyanyaswa, lakini baada ya kifo cha Magufuli, unyanyasaji huo umerudi kama ulivyo.
“Huyu mwekezaji (jina tunalo) ni kama haogopi mtu yeyote sasa, maana mifugo yake inakula mazao yetu, tukilalamika tunaonekana kama hatuna haki. Yaani mazao yetu yamekuwa chakula cha mifugo yake na hakuna anayejali” amesema mmoja wa wakulima hao ambaye kwasababu za usalama, jina lake linahifadhiwa.
Amesema wamelalamika mpaka Wizara ya Ardhi, lakini hawapati majibu ya haraka zaidi ya kuambiwa kwamba suala lao linafanyiwa kazi, huku uongozi wa kata na wilaya ukionekana kumkumbatia mwekezaji huyo anayemiliki ranchi ndogo ya mifugo kijijini hapo.
“Tulikuwa tumeambiwa kwamba aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM, Paul Makonda angefika huku ili kusikiliza kero yetu, lakini baada ya msiba wa Mheshimiwa Edward Lowassa ziara hiyo ikafutwa. Sasa kwakuwa Mheshimiwa Makalla amesema anaanzia pale ambapo Makonda ameishia, tunamwomba aje huku aone namna wanachama wa CCM na wananchi wanavyonyanyasika kutokana na nguvu ya pesa” amesema mwananchi mwingine.
“Huku kuna watu ni jeuri, bendera ya CCM ilichomwa moto na watu hawa, lakini hakuna aliyejali. Wamekuja waandishi hapa, wamechukua picha, lakini wamezidiwa, tajiri analindwa kwa gharama kubwa” amesema mwananchi mwingine.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge hakupokea simu, lakini pia simu ya Mhe. Makalla ilikuwa inaita tu bila majibu.
Lengo la kumpigia RC Kunenge ilikuwa kutaka kujua kama amepata taarifa za mgogoro huo na hatua ambazo amechukua kabla ya madhara kubwa makubwa zaidi, lakini pia mtandao wetu ulikuwa na shauku ya kujua kama Mhe. Makalla atakwenda Kazole kuvalia njuga jambo hilo kama wananchi wanavyomhitaji.