Makao Makuu ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC)
. Shirika kongwe lenye miradi ya kimkakati na mbioni kufufua viwanda vyake
. General Tyre mwekezaji yupo tayari kuweka USD Milioni 120
.Liganga, Mchuchuma wananchi walipwa fidia Tsh bilioni 15.4
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Hapo zamani kulikuwa na kipindi Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) cha Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na kulikuwa na kibwagizo cha ‘sema tena NDC’ na kila ukitembelea maonesho ya sabasaba ni lazima utapita banda la NDC ambalo lipo mwanzoni tu ukiingia viwanja na ukitoka lazima upewe beji yao.
Naam hizo zilikuwa nyakati za NDC enzi hizo miaka 1980 na mwishoni mwa 1990 ni moja ya mashirika makongwe hapa nchini na lilikuwa shirika kubwa enzi hizo ambalo lilikuwa kama kitovu cha viwanda na maendeleo ya uchumi wa nchini kuanzia kilimo , viwanda vya chuma, vioo, karatasi , rangi , vitenge , vinywaji, matairi , vifaa vya umeme na kila aina ya nyenzo za binadamu za maendeleo.
Historia ya NDC inaanza mwaka 1948 ambapo serikali ya kikoloni ya kiingereza kupitia “Overseas Resources Development Act” ya 1948 ilianzisha Colonial Development Corporation- CDC kusaidia makoloni ya Uingereza katika maendeleo ya uchumi.
CDC ilianzishwa kukabiliana na madhara ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na vita ya pili ya dunia na CDC ilipewa majukumu ya msingi ya kuhimiza biashara, kuimarisha uchumi wa kikoloni, kuchochea uzalishaji wa mahitaji ya ndani pamoja na usambazaji wa mahitaji ya nje.
Mwaka 1964, serikali iliboresha Tanyanyika Development Corporation (TDC) kwenye jitihada za utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Kufuatia maboresho hayo, TDC iliongezewa majukumu ikapewa jukumu la kuendesha miradi ya uzalishaji mali katika sekta ya viwanda, kilimo na biashara. Aidha serikali iliielekeza TDC kuwa shirika hodhi au shirika mama na kupewa uwezo wa kumiliki hisa kwenye miradi itakayoidhinishwa na Bodi ya wakurugenzi (“In practical Terms, new TDC will operates as a holding or parent organization)
Akizungumza na Taifa Tanzania kwenye mahojiano maalum kwa njia ya simu kutoka mkoani Dodoma , Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Dkt Nicolaus Shombe alisema NDC bado litaendelea kuwa shirika mama la maendeleo ya nchini na kwa sasa kwenye miradi ya kimkakati na maendeleo ya viwanda hapa nchini.
Aliongeza kwamba shirika linatarajiwa kuwa shirika kiongozi katika kutekeleza malengo ya kimkakati ya kitaifa kwa kuzingatia mazingira ya sasa kwa mfano maendeleo ya teknolojia , mazingira, utandawazi, ushindani, masoko ya mitaji, soko huria na mnyororo wa thamani.
Dkt shombe aliendelea kusisitiza kwamba bado umuhimu wa shirika utaendelea kuwepo katika kusimamia maendeleo ya nchini husika , anarejea kwamba tangu mwaka 1964 baada ya muungano katika hotuba ya Mwl Julius Nyerere Baba wa Taifa kwamba NDC ndio litakuwa na jukumu kubwa wa maendeleo ya viwanda na mpango wa kwanza miaka mitano wa maendeleo lilikuwa jukumu la NDC.
“kufuatia Muungano na kupitia Sheria Na 69 ya mwaka 1964, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliboresha na kubadili Shirika la Maendeleo la Tanganyika (New TDC) na kuanzisha National Development Corporation (NDC)
Aliongeza kwamba kufika mwaka 1969 NDC lilikuwa shirika kubwa ndani ya Afrika Mashariki na Kati kwa maana ya mtaji wa kiasi cha Tsh 571,976,383.00 na makampuni tanzu ambazo lilikuwa linaziendesha kama vile Kibo Match, TBL, Tanalec, UFI, Alaf , Mangula Mechanical,, Tanzania Steel Corporation, Shirika la Madini na mengine mengi.
“Ila baada ya vita vya kagera 1978/79 na mdodoro wa uchumi wa nchini iliundwa Tume ya kurekebisha Mashirika ya Umma kwa hiyo mashirika ambayo yalikuwa yanatengeneza mtaji yakaachwa yajiendeshe kama vile TCC, TBL, Tanalec na mengine yalibinafishwa,” alisema Dkt Shombe
Pamoja na mabadiliko hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa na athari hasi kwa shirika kwa kuliondolea mtaji ila shirika liliendelea kuongoza uhamasishaji wa maendeleo ya viwanda , alisema kwamba kufikia mwanzoni mwa miaka 1990 shirika lilikuwa limeanzisha mashirika mapya ya biashara 12 , mashirika hayo Tanzania Metal Box, Tanzania Cables, Tanzania Light Source Industries, Mbagala Sheet Glass, Nyanza Container Glass, Kilimanjaro Machines Tools Company, National Bicycles Company Limited, Tanga Steel Rolling Mills, Ubungo Farm Implement, Zana za Kilimo Mbeya, Tanalec na Southern Paper Mills.
Alisema kwa sasa kuna miradi kadhaa ya kimkakati ambayo shirika hilo linayasimamia kama vile Liganga , Mchuchuma, Rwegaluka Makaa ya mawe , Ngaka makaa ya mawe , Kilimanjaro Mashine Tools Company na miradi mingine kadhaa ya kimkakati.
Aliongeza kwamba kiwanda cha General Tyre cha Arusha tayari kimepata mwekezaji ambaye yupo tayari kuwekeza katika kiwanda hicho cha matairi kwa kuwela kiasi cha mtaji wa dola za kimarekani 120 Millioni ili kutengeneza miundombinu mipya kwenye kiwanda ili kiwe cha kisasa na kuanza uzalishaji na kutengeneza ajira kwa watanzania.
“kiwanda hiki kina mitambo ya kizamani na miundombinu ya kizamani kwa hiyo mwekezaji ataleta mitambo mipya ya kisasa na teknolojia mpya ya utengenezaji wa matairi nchini na kufungua milango ya ajira kwa watanzania , tupo kwenye mazungumzo ya mwisho kabisa na upembuzi yakinifu umeshafanyika,” alisema Dkt Shombe
Aliongeza kwamba kuhusu kiwanda cha Kilimanjaro Machines Tools Company (KMTC) tayari kimeanza kazi kuzalisha vipuri vya mashine na mitambo mbalimbali mkoani Kilimanjaro.
“serikali kupitia NDC tumejenga tanuru la kuyeyusha chuma lenye uwezo wa kuyeyusha chuma kiasi cha kilo 500 kwa mkupuo mmoja, aliongeza kwamba kwa kukamilika kwa tanuru hilo ni hatua muhimu kwa kiwanda hicho cha Kilimanjaro katika kuzalisha viwanda vingine.
Pamoja na mambo mengine bado serikali imeweza kulipa fidia kwa wananchi kama miradi ya Liganga na Mchuchuma huko Njombe ambapo Tsh 15.4 billioni zililipwa kwa wananchi ili kuweza kupisha mradi huo wa uchimbaji wa makaa ya mawe kama chanzo cha nishati ya umeme hapa nchini.
Aliongeza pia kwamba kupitia eneo lake maalum la kibaha (Kibaha Industria Park) ambapo imegawanyika kwenye sehemu tatu Eneo la utengenezaji magari na vifaa vya magari, sehemu ya madawa na sehemu ya utengenezaji wa nguo , aliongeza kwamba katika eneo la madawa kuna kiwanda cha Kuzalisha bidhaa za kibailojia (TBPL) ambapo kwa sasa wameweza kutengeneza dawa ya kibaiolojia ya kuua mazalia ya mbu na isiyo na madhara kwa viumbe na mazingira.
Alisema kwamba kupitia kiwanda hicho nchini kadhaa za jirani zinategemea kiwanda hicho kuua mazalia ya mbu kwenye nchini zao nchini hizo ni Kenya, Msumbiji, Niger, Angola, Botswana na sasa wanakwenda Zambia hivi karibuni.
Dkt Shombe alisema kwamba anamshukuru mungu kumpa nafasi hiyo nyeti na kuvaa viatu vya Arnold Kilewo, Marehemu Profesa Simon Mbilinyi na Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia ambapo kwa nyakati tofauti wamekuwa Wakurugenzi Watendaji wa shirika hilo kongwe hapa nchini.
Alifafanua kwamba yeye anatokea Wizara ya Fedha , Idara ya Mipango ,Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano alishiriki kikamilifu kuutengeneza na sasa yupo kwenye shirika ambalo linapaswa kutekeleza mipango hiyo ya maendeleo kwa vitendo kwa maslahi mapana ya nchini.