NDICHO unachoweza kusema juu ya kiwango bora alichonacho kiungo mshambuliaji wa Yanga raia wa Ivory Coast, Pacome Zouzoua ‘Zizou’.

Aliposajiliwa, kelele zilikuwa nyingi. Kubwa ni namna alivyoonekana kukwama kuingia kikosi cha kwanza cha Yanga. Akaonekana amefeli.

Leo hii, hakuna anayezungumza vibaya kuhusu Zouzoua. Ametufanya sote tukubaliane kwa sauti moja, kwamba nyota huyo raia wa Ivory Coast ni fundi kweli kweli.

Wapo wanaomtazama kwa takwimu zake za mabao na asisti. Katika maeneo hayo, sidhani kama kuna swali. Anafunga na anatoa asisti za kutosha tu.

Binafsi, nimekuwa nikimtazama kwa jicho la tofauti. Nimekuwa nikifurahishwa zaidi na uchezaji wake na si takwimu za kufunga au kutoa pasi za mabao.

Ndani ya uwanja, Zouzoua ni zaidi ya burudani. Unapotazama uchezaji wake, inakuwa rahisi mno kwako kuamini kuwa soka si mchezo mgumu.

Kwa maana nyingine, uchezaji wake utakufanya ubishane sana na wale wanaoamini kuwa mchezo wa soka ni idadi ya mabao.

Kupitia ufundi wake miguuni, Zouzoua anauongezea thamani mchezo wa soka na kuufanya uwe mzuri zaidi kuutazama.

Unapokwenda kuitazama Yanga yenye Zouzoua ndani ya kikosi, unakuwa umepiga ndege wawili kwa jiwe moja.

Mosi, umekwenda kuiona timu yenye uhakika wa kupata pointi tatu ndani ya uwanja. Pili, umekwenda kufurahia burudani ya soka.

Nilishawahi kusema, soka ni zaidi ya matokeo. Ndani ya soka, kunapaswa kuwapo kwa burudani.
Si kila wakati utahitaji kuona viungo wakigongana katikati ya uwanja. Kuna wakati utatamani kuona pasi za visigino na mbwembwe zingine za aina hiyo.

Hiyo ndiyo kazi anayoifanya Zouzoua. Ndiyo kazi anayoweza kuifanya kwa ufasaha zaidi, labda kuliko hata kufunga na kutoa asisti.

Ulimwengu wa soka haujawahi kukinai kuwaona wachezaji wa aina hii. Leo hii, bado mamilioni ya mashabiki wanamtamani Ronaldinho. Hakuna anayemfikiria David Beckham, Michael Owen wala Thierry Henry.

Unajua sababu? Ronaldinho alifanya hiki tunachokiona kwa Zouzoua. Kuulainisha mpira. Kutofautisha mpira na idadi ya mabao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *