WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Na Mwandishi Wetu
WAKATI viongozi wakuu wa Serikali wakikemea ubadhirifu na kuwataka watendaji wa Serikali hususani kwenye Halmashauri mbalimbali nchini kusimamia vizuri fedha za umma, kuna madai ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za Umma kupitia manunuzi ya Mafuta (Petroli na Diesel) ya magari na vifaa vingine vinavyotumia nishati hiyo yakiwemo majenereta, Wilayani Nanyumbu, Mkoani Mtwara.
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo MorningStarPost limeziona, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu kila mwezi imekuwa ikitengewa Lita 1,200 za mafuta ya Diesel, ambapo Oktoba 14, 2023, Ofisi hiyo ilitumia Lita 295, hivyo ilibaki Lita 905 ambazo matumizi yake hayajulikani.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa Novemba 2,2023 hadi Novemba 30, 2023, matumizi ya mafuta kwenye Ofisi hiyo ya Mkuu wa Wilaya yalikuwa ni Lita 510, hivyo zilibaki Lita 690 za Diesel ambazo nazo hazijulikani zilipo.
Kwa kipindi cha Desemba 1, 2023 hadi Desemba 31,2023, matumizi yalikuwa Lita 630 ya Diesel, ambapo zilibaki Lita 570, na matumizi ya aina hiyo yameendelea hadi Januari, 2024.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nanyumbu (DAS) ambaye miongoni mwa majukumu yake ni pamoja na kuandaa makadirio ya matumizi ya Wilaya, anapata Petroli Lita 300 kila mwezi, lakini matumizi yake hayajulikani.
“Mwandishi wewe umetolea mfano wa miezi mitatu tu na ukiangalia zimepotea zaidi ya Lita 2,165 hiyo ni mbali na zile Lita 300 anazopewa DAS kila mwezi ambazo haijulikani anazitumiaje, lakini mtindo huo umefanyika kwa muda mrefu na bado unaendelea, maana yake ni kwamba Serikali inaendelea kupoteza fedha kupitia manunuzi yasiyo sahihi ya mafuta,” kilisema chanzo chetu cha uhakika (jina tunalihifadhi).
Chanzo hicho kiliendelea kusema, kila mwezi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Katibu Tawala, wamepangiwa kuchukua mafuta kwenye Kituo cha mafuta cha Osam, lakini kiwango cha mafuta kinachotengwa na kinachochukuliwa ni tofauti “Lita zinazotengwa ni nyingi kila mwezi, lakini zinazotumika ni chache, zinazobaki hazijulikani zinakwenda wapi”
“Ukipata nafasi ya kumuhoji DAS na DED (Mkurugenzi wa Halmashauri) waulize yanapokwenda haya mafuta yanayobaki na kama wana nia njema, kwanini hawaweki bajeti kulingana na matumizi? Kama sio ufisadi, kwanini wanaweka bajeti kubwa wakati matumizi yao ni madogo?,” kilihoji chanzo hicho.
Aidha, chanzo hicho kiliweka wazi kwamba, anayepaswa kubanwa na kuchunguzwa kuhusu suala hilo ni DAS, kwani ndiye anayesimamia matumizi na bajeti, “DAS ndiye anayesimamia utendaji wa kila siku wa Wilaya ikiwemo kupanga makadirio ya matumizi, hawezi kukwepa tuhuma hizi.”
Hata hivyo, taarifa zaidi zinadai kwamba, lipo gari aina ya Toyota Probox (namba zake tunazo) ambalo halitumiki, lakini limekuwa likitengewa bajeti ya mafuta ambapo kwa tarehe tofauti kuanzia Desemba 5,2023 limewekewa Lita 225 za mafuta ya Petroli, huku kwa siku tano kuanzia Januari 2, 2024 hadi Januari 11,2024 limewekewa Lita 227 za mafuta.
“Huu ni wizi wa wazi unaofanywa na hawa watendaji ambao wameaminiwa na Rais na wamepewa nafasi ili wawatumikie watanzania na kusaidia jitihada za kuijenga nchi, lakini wao wanatumia vibaya nafasi hizo kufanya ufisadi. Naiomba Serikali na Mamlaka nyingine zinazohusika zije kufanya uchunguzi ili kubaini haya yanayofanyika na huu uwe mfano tu,”
“Wachunguze nchi nzima na hatua zichukuliwe kudhibiti ufisadi wa namna hii, kuna watanzania maskini wanakosa huduma, wengine wanateseka kwa ugumu wa maisha, halafu wapo watu wachache wanachezea fedha kwa matumizi yasiyoeleweka, hizi fedha zinazochezewa huku zingeokolewa zingesaidia maeneo mengine,” kilisema chanzo hicho.
Mwandishi wa habari hizi alimtafuta Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Dkt. Stephen Mwakajumilo kupitia simu yake ya mkononi bila mafanikio, na taarifa ambazo zilipatikana baadae, ilidaiwa yupo kwenye kikao, ingawa jitihada zaidi za kumtafuta zinaendelea.
Alipotafutwa Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu (DED) Ibrahim Mwanauta kupitia simu yake ya mkononi na kuulizwa kuhusu utaratibu unaotumika kwa mafuta yanayobaki iwapo yametumika chini ya kiwango kilichotarajiwa, alimtaka mwandishi wa habari hizi kumtafuta DAS, kwani ndiye anayeweza kutoa ufafanuzi wa suala hilo “hizi ni ofisi mbili tofauti, mtafute DAS.”
Hata hivyo, alipotafutwa Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Juma Said Kanyinda, alisema anahitaji muda wa kufuatilia suala hilo, ingawa aliweka wazi kwamba mafuta ambayo wanapewa kwa ajili ya majukumu yao wakati mwingine yanakuwa hayatoshi, kwani kuna kipindi yanatumika zaidi hususani wakati wa ziara.
Kayinda aliendelea kusema kuwa, mbali na matumizi hayo wakati wa ziara, wamekuwa wakitoa mafuta kwa Idara nyingine wakiwemo Jeshi la Polisi Wilayani humo, na kuhusu madai ya gari aina ya ‘Probox’ ambalo linadaiwa kutengewa mafuta wakati halitumiki, alisema linatumika na alipotakiwa kujibu linatumika kwa shughuli gani, alimjibu mwandishi kwamba ‘wewe sio mtu sahihi wa kuniuliza hilo swali.’
Waandishi wa MorningStarpost wanaendelea kufuatilia zaidi suala hilo Wilayani Nanyumbu na maeneo mengine nchini, kwani zipo taarifa kwamba maeneo mengi mtindo huo unafanyika jambo ambalo linasababisha hasara kubwa kwa Serikali.