Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mhe. Isaack Mwakajumilo akiwa kwenye picha ya pamoja na wakazi wa Nanyumbu baada ya kusimikwa kama kiongozi wa heshima na kuwa Mwenye wa kabila la Wamakua kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru yalifanyika wilayani humo,
Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara, Mhe. Isaack Mwakajumilo, amewataka watumishi wa afya kuacha kuomba rushwa wakina mama wajawazito wanaofika kwenye zahanati.
Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru, kwenye Kituo cha Afya Mikangaula katika Halmashuri ya Wilaya ya Nanyumbu Kata ya Mikangalua mkoani Mtwara.
Akizungumza kwenye sherehe zilizilizotanguliwa kwa kufanya shughuli mbalimbali katika kata hiyo, Mhe. Mwakajumilo alisema wakina mama wengi wajawazito wanaogopa kufika kwenye vituo vya afya kuhofia kuombwa rushwa.
“Fahamu kuwa wakina mama wengi wajawazito hawafiki kwenye vituo afya, wengi wanahofia kuombwa pesa na wahudumu wa vituo hivyo, kwa hivyo muache mara moja kufanya hivyo, tunataka katika wilaya hii tufike mahali tuwe na takwimu za wamama wajawazito” alisema Mhe. Mwakajumilo.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya ametuma salamu za pole kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maafa yaliotokana na maporomo kwa wananchi wa Katesh.
Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa wilaya hiyo aliongoza wakazi wa kata hiyo kupanda miti ya matunda na kufanya usafi maeneo mbalimbali na kukabidhi vifaa tiba vilivyotolewa na serikali katika kituo cha afya cha Mikangaula.
Alisema upandaji wa miti ya matunda utasaidia wakazi wa maeneo hayo kupata matunda na wakati huo huo kupata kivuli.
Katika hatua nyingine, viongozi wa kimila wakiongozwa na Mwenye Kawaki ambaye ni makamu wa kiongozi wa kabila la Wamakua walimsimika mkuu huyo wa wilaya kuwa Mwenye ambaye ni kiongozi wa heshima wa kabila la hilo.
Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu, Mhe. Isaack Mwakajumilo akipanda miti katika maadhimisho ya sherehe za uhuru yaliofanyika katika kituo cha afya cha Mikangalula wilayani Nanyumbu.