Na MWANDISHI WETU
Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji Kampuni ya AFCONS INFRASTRUCTURE LTD, ameingia kwenye shida kubwa baada ya kutakiwa na mkuu wa wilaya ya Nanyumbu kuhakikisha wanachunguzwa na kuona uhalali wao wa kuendelea na mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mkoa Mtwara Isack Mwakajumilo, amewaagiza uhamiaji kuchunguza vibali vya kuishi vya wafanyakazi na viongozi wa kampuni hiyo ya mradi huo wa maji baada ya kutilia mashaka utendaji wao.
Mkuu wa wilaya Mwakajumilo alitoa maagizo hayo baada ya kutembelea ujenzi wa mradi wa maji Ruvuma na kubaini mapungufu mengi ambayo yamempa mashaka makubwa kuhusu utekelezaji na uhalali wa mkandarasi huyo kufanya kazi katika mradi huo.
Baada ya kutembelea mradi huo, Mkuu wa wilaya alibaini kuwa ofisi ya mkandarasi anayefanya ujenzi huo badala ya site ya mradi kuwa karibu na eneo la Masuguru imewekwa kilometa 70 kutoka mradi huo ulipo hatua ambayo inadhorotesha utendaji wa mradi huo.
“Leo nimeenda kukagua wajenzi wa mradi wa maji wa Ruvuma na kubaini yafuatayo Ofisi iko Mangaka badala ya site huko Masuguru km.70 toka mjini Ofisi yenyewe haina bango lolote la kuonyesha ofisi ilipo. Tangu project imeanza hadi Sasa imefikisha 2.74% pamoja na kupewa sh.5.6 bilioni” alisema Mwakajumulo
Pia, tangu mradi huo umeanza mpaka sasa imefikia asilimia 2.74 ya utekelezaji na wamebakiwa na miezi 13 wa kutakiwa kukabidhi mradi huo.
Mkuu huyo wa wilaya alipowataka wakandarasi hao kumpa profile ya mradi wa kampuni yao walishindwa.
Mkataba wa mradi wa ujenzi wa mradi huo ni miezi 20 mpaka sasa imepita miezi saba wamebakiwa na miezi 13 mradi kukamilika.
“Nimewaagiza uhamiaji kesho waende wakakague vibali vyao vya kazi uhalisia wa wenyewe kuendelea kubaki nchini, hati zao za kusafiria uzoefu wao katika kazi nakadhalika, alisema Mkuu wa wilaya.
Mkuu wa wilaya Mhe. Mwakajumulo akiwahoji viongozi wa kampuni ya mradi wa ujenzi Ruvuma ofisini kwao