Na Mwandishi Wetu

Idara ya Uhamiaji Nchini, imelalamikiwa kuweka gharama kubwa ya kulipia hati ya kusafiria iwapo itapotea.

Akizungumza na Morningstar POST, Mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Bw. Jackson Kashinde, alisema kuwa sheria hii mpya inapaswa kuangaliwa upya kwa kuwa inawabebesha mzingo mkubwa watu ambao wamepoteza hati ya kusafiria kwa bahati mbaya.

“Sisi ni binadamu unaweza ukawa makini kutunza ”Passport” lakini kutokana na majanga ya moto au hali isiyo ya kawaida ikatokea umepoteza inakuwaje utozwe gharama mara tatu ya gharama ya awali ya kulipia “passport”, alisema Kashinde.

Akizungumzia suala hilo, Mkazi wa Mbezi Luis , Mashaka Ingondea alisema kuwa hakubaliani na sheria hiyo kwa kuwa haikulitazama suala hilo kwa makini kwa kuwa kupoteza kitu sio kitu cha hiari.

Alisema kuwa ni kweli tunapaswa kuwa makini kutunza hati zetu lakini suala la kupotea haliepukiki lazima inaweza kutokea ukapoteza kwa nini mzigo mkubwa uende kwa mtu aliyepoteza tu? Alihoji.

Msemaji Mkuu wa Idara hiyo Paul Mselle, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, kinachoruka kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa, saa 12:00 Asubuhi hadi saa 4:00 Asubuhi, alisema kuwa uwepo wa ulazima wa faini hiyo umesaidia hata kesi za watu kupoteza passport zao kupungua.

“Passport siyo kwamba ni kitambulisho mtu anatakiwa awe nacho akaweke ndani, kwa sababu passport ukiipoteza gharama yake ni kubwa sana ili kuipata nyingine, sasa hivi kuipata hii ya kawaida ni 150,000, lakini ukipoteza utalazimika kulipa Laki Tano kwa kupoteza hiyo passport, wameiweka hiyo ili kuweka udhibiti na mtu aweze kuitunza,” ameeleza Mselle

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *