Na Mwandishi Wetu
Ikiwa imepita takribani miezi nane tangu Said Hussein Massoro ateuliwe kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan jana alifanya mabadiliko na kumteua Balozi Ali Idi Siwa katika nafasi hiyo.
Massoro aliteuliwa kushika nafasi hiyo Januari 3 mwaka huu na kudumu kwenye ofisi hiyo nyeti kwa miezi nane kabla ya kuteuliwa kuwa balozi.
Kabla ya kupewa jukumu hilo Massoro alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu na Mkurugenzi wa Shughuli za Ndani wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imeeleza kuwa Balozi Siwa aliapishwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam tayari kuitumikia nafasi hiyo nyeti na muhimu kwa Usalama wa Taifa.
Kabla ya uteuzi huo Balozi Siwa alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) nafasi aliyohudumu tangu Septemba 20, 2018.
Kabla ya hapo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda kwa takribani miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2018.

Siwa Mkurugenzi Mpya Usalama wa Taifa