Na Aloyce Kulwa

Miili 12 kati ya 13 iliyokuwa imezama ndani ya Ziwa Victoria imeopolewa hadi kufika saa 1 asubuhi leo Jumatano Agosti 2, 2023.

Idadi hiyo inafikisha jumla miili 13 kuopolewa kutokana na tukio hilo lililotokea wakati watu hao wakitoka katika kijiji cha Mchigondo kwenda Kitongoji cha Bulomba katika Kijiji cha Igundu baada ya mwili wa mtoto wa mwaka mmoja kuopolewa siku ya tukio.

Jana Agosti Mosi 2023 miili miwili ilikuwa imeopolewa ziwani ambapo wote walikuwa ni watoto wa kike.

Miili mingine imeopolewa kati ya usiku hadi leo Agosti Mbili saa moja asubuhi.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara,  Agostino Magere amesema vikosi vya uokoaji kwa kushirikiana na wavuvi  na wenyeji eneo hilo wanaendelea kuutafuta mwili mmoja ambao umesalia.

Julai 30, 2023 mitumbwi miwili iliyokuwa imebeba waumini 28 wa Kanisa Takatifu la Mungu wa Kiroho (KTMK) ilizama ziwani ambapo watu 14 waliokolewa na kukimbizwa hospitalini.

Katika tukio hilo ambapo wengi walikuwa ni watoto na wanafunzi wa Shule ya Msingi Bulomba wilayani Bunda, watu 13 walizama ambapo shughuli ya kuwatafuta ilianza hadi sasa ambapo bado mwili mmoja.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *