Na Washirika Wetu
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeanzisha uchunguzi baada ya barua pepe zenye taarifa za siri kutumwa kwa mshirika wa karibu wa Urusi kutokana na kosa la kimaandishi.
Barua pepe hizo zilikusudiwa kutumwa kwa jeshi la Marekani, ambalo linatumia jina la siri la “.mil”.
Lakini walisahau herufi ‘i’, na hivyo ujumbe ulikwenda badala yake katika taifa la Afrika Magharibi la Mali.
Maafisa wa ulinzi wanasema barua pepe hizo hazikuwa na habari zinazoweza kuathiri usalama wa utendakazi.
“Tumeanzisha uchunguzi baada ya idadi ndogo ya barua pepe kutumwa kimakosa kwenye barua isiyo sahihi,” msemaji wa Wizara ya ulinzi ya Marekani aliliambia shirika la habari la PA. “Tuna uhakika hawakuwa na taarifa yoyote ambayo inaweza kuathiri usalama wa uendeshaji au data ya kiufundi.”
Msemaji huyo aliongeza kuwa taarifa zote nyeti zinazotumiwa na idara ya serikali “zilishirikishwa kwenye mifumo iliyoundwa ili kupunguza hatari ya upotoshaji”.
“Wizara ya ulinzi mara kwa mara hukagua michakato yake na kwa sasa inafanya mpango wa kazi ili kuboresha usimamizi wa habari, kuzuia upotevu wa data, na udhibiti wa habari nyeti,” msemaji huyo alisema.
Mapema mwezi huu, iliibuka kuwa mamilioni ya barua pepe za kijeshi za Marekani pia yalitumwa nchini Mali, kwa sababu za hitilafu sawa ya uandishi.
Baadhi ya barua pepe hizo ziliaminika kuwa na taarifa nyeti zikiwemo nywila, rekodi za matibabu na ratiba za maafisa wakuu.
Mali ilikuwa moja ya nchi sita za Kiafrika zilizoahidiwa kupelekewa nafakab bila malipo na Rais wa Urusi Vladimir Putin baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya Bahari Nyeusi na Ukraine mapema mwezi huu.
Jeshi la wanamaji la Urusi lilizuia bandari za Bahari Nyeusi za Ukraine kufuatia uvamizi wake Februari 2022, na kukamata tani milioni 20 za nafaka ambazo zilikusudiwa kuuzwa nje ya nchi na kusababisha uhaba wa chakula katika nchi za Mashariki ya Kati na Afrika.
Mali pia ni mshirika wa karibu wa Urusi kwa sababu mamluki wa Wagner wa Moscow wametumwa nchini humo kupigana pamoja na jeshi dhidi ya wanajihadi.
Mapema wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema waziri wa ulinzi wa Mali, mkuu wa jeshi la anga na naibu mkuu wa majeshi watawekewa vikwazo kwa kuratibu uenezi wa Wagner katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
.
Rais wa Marekani Bw. Joe Biden