Na Mwandishi wetu
Siku chache baada ya polisi kuvamia nyumba ya mwanawe Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta, Jomo, Mkuu huyo wa zamani wa nchi kwa mara nyingine amezungumza kuhusu kisa hicho akidai kuwa kulikuwa na mpango wa kumwekea bunduki na dawa za kulevya wakati wa operesheni ya Ijumaa usiku.
Wakati wa mkutano na wahariri wa habari mnamo jana Jumatatu, Bw Kenyatta pia alizungumzia madai ya kuhifadhi bunduki zinazodaiwa kushikiliwa na wanawe wawili, Jomo na Muhoho.
“Suala hili la bunduki limezingirwa na propaganda nyingi ili kugeuza mawazo kutoka kwa kile ambacho kimekuwa kikitokea nchini,” aliwaambia waandishi wa habari
“Ninaamini walitaka kuweka dawa na bunduki katika boma la mwanangu.”
Kenyatta aliyejawa na hasira anasema tukio hilo lilimuumiza.
“Nilienda kwa sababu ya simu ya dhiki kutoka kwa mwanangu; sikuwa mlevi, niliumia sana,” alisema.
Rais huyo wa zamani anadai kuwa wanawe wawili wanamiliki bunduki sita kwa jumla, tatu kila mmoja, na kwamba bunduki zote zimesajiliwa kisheria. Alifafanua kuwa binti yake Ngina hamiliki bunduki.
Kulingana na Rais huyo wa zamani, hakuna hata mmoja wa wanawe ambaye amepokea amri ya kusalimisha silaha zake kama inavyodaiwa kwenye vyombo vya habari na maafisa wakuu wa serikali.
Baada ya uvamizi wa nyumba ya mtoto wa rais huyo wa zamani ,serikali ilithibitisha kuvamia nyumba tatu katika eneo la Karen jijini Nairobi kutafuta bunduki 23 zinazodaiwa kutumika kutekeleza operesheni haramu nchini wakati wa maandamano ya kuipinga serikali .
Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema vyombo vya usalama vimepewa jukumu la kupekua eneo hilo kama sehemu ya operesheni pana inayolenga kuwaondoa watu walio na silaha na viongozi wa magenge ya uhalifu yanayojulikana.
Kenyatta pia alifichua kuwa amelazimika kushiriki usalama wake na mamake, Mama Ngina Kenyatta, baada ya usalama wake kuondolewa wiki jana.
“Faida ambazo mama yangu anapata si kwa sababu yangu bali kwa sababu yeye ni Mama wa Kwanza wa zamani,” alisema.
“Tumelazimika kuajiri walinzi wa kibinafsi.” rais huyo wa zamani amesema
Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta