Na Happyness Hans,

WAF, Dar es Salaam

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Kupambana na Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Ezron Nonga, amesema Kongamano la 17 la Chuo Kikuu la Uwasilishaji na Uenezi wa Matokeo ya Tafiti limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa lengo la kuwasilisha matokeo ya tafiti kuhusu usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa binadamu na wanyama.

Amesema hayo katika Chuo kikuu cha afya na Sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam. Amesema Serikali imeunda kamati maalumu inayoshirikisha sekta mbalimbali za afya ili kuratibu mapambano dhidi ya usugu wa vimelea, tatizo ambalo limekuwa likiongezeka na kuathiri afya ya jamii.

Kwa mujibu wa Profesa Nonga, amesema juhudi zinazofanywa kupitia kamati hiyo zimechangia kupungua kwa matumizi holela ya antibiotiki, maambukizi yanayohusishwa na usugu wa dawa pamoja na vifo vinavyotokana na tatizo hilo. amesema kuwa, wafugaji wameendelea kuhamasishwa kuzingatia ufugaji bora na usafi ili kudhibiti magonjwa kwa wanyama.

Ameongeza kuwa kampeni ya “Holela Holela Itakucost” imewafikia zaidi ya watu milioni 24 hapa nchini na kuwapa elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa, huku akiwataka wananchi kuacha kujitibu wenyewe na badala yake watumie dawa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuimarisha mapambano dhidi ya usugu wa vimelea kwa dawa.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Erasto Mbugi, amesema jukumu kuu la Taasisi hiyo ni kufundisha, kufanya tafiti na kutoa huduma za afya, hivyo suala la usugu wa vimelea ni sehemu muhimu katika kuboresha huduma za matibabu nchini.

Amesema,MUHAS imeendelea kufanya warsha na tafiti mbalimbali ili kuwajengea uwezo wanafunzi, madaktari na watoa huduma za afya katika kukabiliana na usugu wa vimelea, huku ikiendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu hatari ya maambukizi yanayoweza kutoka kwa wanyama na namna ya kujikinga nayo.

Naye mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Microbiology katika MUHAS, Lilian Kyone, amesema kongamano hilo limewapa wanafunzi na watafiti chipukizi fursa ya kuelewa kwa kina ukubwa wa changamoto ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa na kuwajengea uwezo wa kufanya tafiti pamoja na kuelimisha jamii ili kuchangia kudhibiti tatizo hilo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *