Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mwenyeji wake, Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame, wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Rwanda, yenye lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano katika sekta ya nishati ya umeme, mafuta, gesi asilia pamoja na kufanya biashara ya nishati ya umeme kati ya Mataifa hayo mawili.
Aliyesaini Hati hiyo kwa niaba ya Tanzania ni Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), na Rwanda iliwakilishwa na Waziri wa masuala ya Miundombinu, Mhe. Dkt. Jimmy Gasore.
Makubaliano hayo yanaweka bayana namna Tanzania na Rwanda zitakavyoshirikiana katika ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme itakayounganisha Tanzania na Rwanda na hivyo kuwezesha biashara ya kuuziana umeme.
Ushirikiano huo utahusisha pia utafutaji, uchimbaji na usafirishaji wa mafuta na gesi asilia na uendelezaji wa miundombinu ya uhifadhi wa Mafuta.
Tukio hilo limefanyika Kando ya Mkutano wa Pili wa Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kigali, nchini Rwanda.
Masuala mengine yatakayosimamiwa katika makubaliano hayo ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya kikanda ya umeme ikiwemo mradi wa Rusumo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 80 pamoja na mradi wa Nsongezi unaotarajiwa kuzalisha megawati 39 katika Mto Kagera.
Tukio hilo pia limeshuhudiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmood Thabit Kombo (Mb), Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mhe. Seif Kombo Pandu.
Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Dkt. Habib Kambanga, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Wizara ya Nishati, Mhe. Innocent Luoga, pamoja na wataalam wengine kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.