Serikali imesisitiza kuendelea kuimarisha na kuboresha mazingira ya kuwajengea uwezo wasichana katika matumizi ya teknolojia zinazoibukia, ikiwemo Akili Unde (AI), ili kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe Dkt. Switbert Zacharia Mkama(Mb), wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Mkama (Mb.), amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wasichana kushiriki kikamilifu katika TEHAMA na kunufaika na fursa za ajira pamoja na ubunifu wa kidijitali.
Amesema TEHAMA imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuwahamasisha wasichana kujikita katika masomo ya Sayansi, Teknolojia Uhandisi na Hisabati yaani STEM ili kupunguza pengo la kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uchumi wa kidijitali.
Maadhimisho hayo yameongozwa na kaulimbiu isemayo, “Akili Unde kwa Maendeleo: Wasichana Wakichagiza Mustakabali wa Kidijitali,” yenye lengo la kuwajengea wasichana ujuzi wa teknolojia za kisasa, kuongeza ubunifu na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.