Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kuimarisha mfumo wa afya nchini na kufanikisha azma ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wote.

Akifungua Kongamano la Wadau wa Sekta Binafsi ya Afya Aprili 20, 2026 jijini Dodoma, kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Samizi amesema takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 50 ya matumizi ya afya nchini yanachangiwa na sekta binafsi.

Amesema pia takribani asilimia 40 ya vituo vya kutolea huduma za afya vinamilikiwa au kuendeshwa na sekta hiyo, hali inayoifanya kuwa mshirika wa kimkakati katika utoaji wa huduma na ajira kwa wataalamu wa afya.

Amebainisha kuwa pamoja na mafanikio yaliyopo, bado kuna umuhimu wa kuongeza nguvu katika huduma za kinga ili kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari, saratani na magonjwa ya moyo.

Dkt. Samizi amewataka wadau wa sekta binafsi kuwekeza zaidi katika uchunguzi wa mapema, elimu ya afya kwa jamii na programu za kubadili tabia hatarishi ili kupunguza gharama za matibabu na madhara kwa wananchi.

Aidha, amesisitiza uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu katika utoaji wa huduma za afya, akionya kuwa sekta hiyo inabeba dhamana ya maisha ya watu na hivyo inapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *