Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Reuben Kwagilwa (Mb), amezuia ombi la kuongezewa muda wa mwaka mmoja kwa kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering Group Corporation Ltd ya China inayotekeleza ujenzi wa barabara za Oljoro, Engosheratoni na Olasiti zenye jumla ya kilomita 10.23, na badala yake kuagiza iongezwe miezi minne kama ilivyopendekezwa na Mhandisi Mshauri.

Mhe. Kwagilwa ametoa uamuzi huo baada ya kupokea tathmini ya Mhandisi Mshauri kampuni ya Consultancy Ltd, ambaye amesema wamefanya uchambuzi wa kina na kuwasilisha mapendekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya kuongeza muda wa miezi minne ili mkandarasi amalize kazi zilizosalia.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo Januari 19, 2026, Mhe. Kwagilwa amesema “Hakuna habari ya mwaka mzima, yaani kazi ya mwaka mmoja unaomba tena extension ya mwaka mmoja, hicho alichoshauri mhandisi mshauri cha miezi minne ndiyo hicho fanyieni kazi,” amesema Mhe. Kwagilwa.

Mradi huo ulianza Novemba 20, 2023 na ulitarajiwa kukamilika Desemba 31, 2025 na hadi sasa umefikia asilimia 86 ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji, barabara ya Oljoro yenye urefu wa kilomita 1.745 imekamilika ujenzi wa daraja na uwekaji wa tabaka la C1 unaendelea. Barabara ya Engosheratoni tayari imewekwa lami kwa kilomita 4.3, zimefungwa taa 110 na ujenzi wa mitaro unaendelea.

Kwa upande wa barabara ya Olasiti, kilomita 2.5 tayari zimewekwa lami, zimefungwa taa 133 na ujenzi wa mitaro unaendelea, huku Naibu Waziri akisisitiza kazi ikamilike kwa muda uliopendekezwa bila kuathiri ubora wa mradi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *