Jengo la China Enterprises Trading Limited ambalo nyuma yake unaendelea ujenzi ambao unadaiwa kukiuka taratibu za ujenzi
Na Anania Njonjo
KUFUATIA habari ambayo mtandao huu iliandika siku chache zilizopita kuhusu kampuni ya China Enterprises Trading Limited iliyopo Kitalu namba 107, Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam ambayo inadaiwa kukiuka taratibu mbalimbali za ujenzi na ukwepaji mkubwa wa kodi, vyombo mbalimbali vya dola vimeanza uchunguzi kuhusu tuhuma hizo.
Awali, MorningStarPost iliripoti kwamba, Kampuni hiyo ambayo inamilikiwa na raia kutoka China, ipo kwenye hatua za ujenzi wa jengo la ghorofa tatu, nyuma ya jengo lao lasasa, huku ikielezwa kuna zuio kutoka kwa Mamlaka ya Mipango Miji, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Kampuni hiyo inadaiwa ilizuiwa kujenga jengo hilo hadi watakapobadilisha ramani yao kutoka ghorofa tatu hadi mbili ambazo zinaruhusiwa kutokana na eneo husika.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wetu umebaini kuwa, wamiliki wa kampuni hiyo wamekahidi agizo la mipango miji la kusimamisha ujenzi, na badala yake wanaendelea kujenga kwa kutumia ramani yao ya awali ya ghorofa tatu, huku ikidaiwa wanawatumia mafundi wa kawaida badala ya kutoa tenda kwa kampuni inayotambuliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).
Aidha, taarifa zilizopo zinadai kwamba, kampuni hiyo inatekeleza ujenzi huo bila kuusajili Bodi ya Wahandisi (ERB) Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi AQRB.
Mbali na tuhuma hizo, inaelezwa kwenye mradi huo kuna ukwepaji mkubwa wa kodi ambapo wahusika hawajaingia mikataba na wakandarasi wanaotambulika hivyo wanaikosesha Serikali mapato, pia hawana mikataba na wafanyakazi, hivyo kuhatarisha maisha ya wafanyakazi hao ambao hawajasajiliwa WCF (Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi), NSSF (Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii) na OSHA (Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi).
Kutokana na tuhuma hizo, mmoja wa waandishi wa mtandao huu alitafutwa na mtu aliyejitambulisha ni mtumishi wa taasisi (tunaihifadhi kwasasa) akiomba ushirikiano wa baadhi ya taarifa kwa ajili ya kuwasaidia kwenye uchunguzi wao.