……. Zinatoa matibabu bila madaktari waliothibitishwa

…….. Dawa zao hazina maelekezo ya matibabu kwa wagonjwa

……… Mifumo ya malipo ya matibabu yajaa ukwepaji wa kodi

Na Waandishi Wetu

KUZAGAA kwa zahanati zinazotoa tiba ambazo zinamilikiwa na raia wa Korea Kaskazini hapa nchini, kumenasibishwa na bomu hatari ambalo Tanzania kama taifa tumelikalia.

Uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa na wanaharakati huru umegundua kuwepo kwa uholela wa utoaji wa matibabu ambao unafanywa na zahanati hizo, huku kukiwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi katika uendeshaji wa zahanati hizo.

Uchunguzi huo umebainisha kuwa asilimia kubwa ya zanahati hizo zinaendeshwa huku zikiwa zimekiuka Sheria, kanuni, na miongozo mbalimbali ikiwemo Sheria ya Hospitali za Kibinafsi,

Sheria ya Famasia ya 2011, Sheria ya Baraza la Tiba la Tanzania, Sheria ya Usajili wa Maabara za Afya Binafsi (Sheria ya Usajili) Sura ya 136 ya Mwaka 2023, na Sheria ya Hospitali Binafsi SURA 151.

Nyingine ni pamoja na Sheria ya Dawa na Sumu SURA 219, Sheria ya Dawa na Vifaa vya Tiba SURA 219 (Ya Mwaka 2021), Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya Tanzania ya 2003, Sheria ya Famasi Kanuni ya 2011 GN 301/2012 na miongozo kuhusu umbo na maudhui ya lebo za bidhaa za matibabu.

Hata hivvo, pamoja na uwepo wa sheria na kanuni hizo, uchunguzi umebaini kuwepo kwa uvunjifu mkubwa wa kisheria unaofanywa kwa makusudi jambo ambalo ni hatari kwa afya za watanzania na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Uchunguzi huo umeonesha kuwa katika baadhi ya zahanati hizo kwenye Wilaya za Kinondoni, Ubungo na Temeke mkoani Dar es Salaam kuna uvunjifu mkubwa wa Sheria za nchi.

Mgonjwa mmoja aliyepata tiba katika moja ya zahanati hizo (jina tunalihifadhi) alilalamika kuhusu dawa zilizotolewa na kliniki hizi.

Alilalamika kwamba dawa alizopewa na kliniki hiyo licha ya kuzinunua kwa gharama kubwa, lakini zimemletea madhara makubwa kiafya ikiwemo kuharisha kwa muda mrefu, kutapika na kuvimba miguu, na hajapata nafuu ya ugonjwa ambao umempeleka kwenye zahanati hiyo.

Amesema kwamba kibaya zaidi ni kwamba dawa hizo zimeandikwa kwa lugha ya Kikorea jambo ambalo amesema limemuwia vigumu kujua hata maelekezo yake, lakini pia kufahamu muda sahihi wa ukomo wa matumizi yake.

“Nimeambiwa kwamba hawa wanaoendesha Zahanati hizi ni raia wa Korea Kaskazini na wameandika dawa hizo kwa lugha ya kwao. Swali langu ni kwamba mbona dawa katika hospitali zetu za serikali kutoka katika nchi hiyo na nchi nyingine zimeandikwa kwa Kingereza?”, amehoji mwananchi huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wapigania Uzalendo Tanzania, Saidi Othman Mohammed amesema kwamba kuna haja sasa Mamlaka husika kwa maana ya Wizara ya Afya kutoa kauli na utaratibu ambao utaondoa mashaka kuhusiana na janga hili.

Amesema nyingi ya Zahanati hizo zipo katika mazingira ambayo hayana hadhi ya Zahanati kwa maana ya nyumba zilizokodishwa kuendesha zahanati hizo, lakini hata madaktari wenyewe wanaotoa tiba wanaonekana kama hawana ujuzi wa kutosha na kama wamethibitishwa na Mamlaka husika.

“Madaktari wanaofanya kazi katika kliniki hizo hawatoi dawa kwa wagonjwa; kwa kawaida huziandika katika vitabu vyao vya kaunta, hawana karatasi rasmi ya dawa, kinyume na sheria na taratibu za matibabu. Mazingira ya maabara hayafai, ni machafu, na hayafikii viwango vya matibabu” amesema na kuongeza;

“Dawa hutolewa kwa wagonjwa bila kuonesha ni aina gani ya dawa, na itatumikaje, jina la daktari au muuguzi anayetoa dawa halioneshwi, Dawa nyingi zinazotolewa kwa wagonjwa hazina majina, na nyingi zimeandikwa kwa lugha ya kigeni, si Kiswahili wala Kiingereza, kinyume na sheria zinazosimamia dawa lakini pia Wagonjwa hawapewi risiti ya kodi baada ya kupata huduma hizo”.

Amesema serikali ifanye ukaguzi na kutoa maamuzi kwasababu katika zahabari hizi hawatoi risiti ya EFD, na kwa kawaida huchukua malipo ya pesa taslimu, akisema kwamba Wakorea hao wanakwepa kodi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kama Taifa ni kama tumejitegea wenyewe bomu hatari kwa afya na uchumi wetu.

“Kwanini tunaruhusu afya za Watanzania kuchezewa? Ukifika katika zahanati hizi kuna madudu mengi. Vitanda vingi vya wagonjwa vimetengenezwa kwa mbao, na baadhi yake viko katika hali mbaya. Hata mazingira ya hospitali si mazuri. Baadhi ya vibali vyao vya uendeshaji wa matibabu vimemalizika muda wake, Dawa zao nyingi hazina Ofisi ya Viwango (TBS), lakini pia hakuna utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa” amesema.

Kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Sumu, Sura ya 219, na Sheria ya Chakula na Dawa na Vipodozi ya Tanzania ya 2003, dawa lazima ziandikwe kwenye makasha yao kwa Kiingereza au iliyoandikwa kwa Kiswahili.

Lakini uchunguzi umeonyesha kuwa dawa ambazo zinatolewa na Wakorea hao hazina jina la mtengenezaji, hazina tarehe za mwisho wa matumizi,hazina nembo ya TBS, Dawa zote ziko katika mfumo wa vidonge, zote ziko katika lugha ya kigeni na hazioneshi zilikotoka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *