MKOA wa Iringa umeendelea kung’ara ndani ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kupitia ubunifu na kasi ya utekelezaji wa mradi wa jengo la kisasa la Iringa Commercial Complex, unaojengwa eneo la Gangilonga, Manispaa ya Iringa.

Mradi huo, unaojumuisha maduka ya biashara, ofisi na nyumba za makazi, umevutia hisia za pongezi kutoka kwa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC, baada ya kujionea hatua zilizofikiwa katika ujenzi unaoendelea kwa kasi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Eliud Sanga, alisema mradi wa Iringa Commercial Complex ni kielelezo cha dira ya Shirika ya kujitegemea kifedha kupitia uwekezaji wa majengo ya kibiashara yanayoendana na mahitaji halisi ya soko.

“Mradi huu ni ushahidi wa namna NHC inavyobadilika na kwenda na wakati. Unatoa fursa kwa wananchi kupata maeneo ya biashara na makazi katika mazingira salama na ya kuvutia, huku ukiinua mapato ya Shirika,” alisema Bw. Sanga.

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa Iringa, Bi. Esther Magese, alibainisha kuwa mradi huo umelenga kujibu mahitaji makubwa ya makazi na maeneo ya biashara katika mkoa huo unaokua kwa kasi.

“Tumeona fursa kubwa katika ongezeko la shughuli za kiuchumi mkoani Iringa, hivyo mradi huu ni jibu la mahitaji hayo. Tunatarajia mapato ya Shirika kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 kutokana na uwekezaji huu,” alisema.

Bi. Magese aliongeza kuwa miradi kama hii inaimarisha hadhi ya NHC katika mikoa, huku ikionyesha dhamira ya Shirika kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora, salama na yenye thamani ya uwekezaji.

Bodi ya Wakurugenzi ilipongeza Mkoa wa Iringa kwa kuwa miongoni mwa mikoa inayoonyesha ubunifu na matokeo halisi ya mikakati ya kuongeza mapato, na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika miradi ya kimkakati ya aina hiyo.

Mradi wa Iringa Commercial Complex unatarajiwa kuwa kitovu kipya cha biashara na makazi ya kisasa katika nyanda za juu kusini, ukiibua fursa za ajira, kuongeza mzunguko wa fedha na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Iringa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *