Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uzinduzi wa miradi mikubwa mitatu katika eneo la Kwala, Wilaya ya Kibaha ikiwa ni pamoja na Bandari Kavu ya Kwala, huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa reli ya kisasa (SGR), na uwekaji wa jiwe la msingi kwa Kongani ya Viwanda ya Kwala.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema miradi hiyo inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara, viwanda na usafirishaji Afrika Mashariki.
Ameelekeza huduma zote za kibandari zihamie Kwala ifikapo Agosti 4, 2025, huku akihimiza sekta binafsi kuchangamkia fursa zilizopo na kutumia miundombinu ya reli kuongeza tija.
Akizungumza kwenye hafla hiyo waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amesema zaidi ya viwanda 200 vinatarajiwa kujengwa kwa uwekezaji wa zaidi ya Dola bilioni 3 na mauzo yake kwa mwaka itakuwa dola bilioni 6 na kuleta ajira zipatazo 250,000 zikiwemo 50,000 za moja kwa moja kwa vijana wa Mkoa wa Pwani.
Uzinduzi wa miradi hiyo umehudhuriwa pia na Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na amesema ajira zitakazozalishwa zitazidi hata idadi ya watu katika baadhi ya miji ya Pwani, jambo linalodhihirisha athari chanya za mradi huo kwa wananchi.